Amnesty: Maisha ya raia wa al Hudaidah, Yemen yamo hatarini
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49358-amnesty_maisha_ya_raia_wa_al_hudaidah_yemen_yamo_hatarini
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mapigano makali yanayoendelea katika mkoa wa al Hudaidah huko kwenye pwani ya magharibi mwa Yemen na kusema kuwa, maisha ya raia katika eneo hilo yanakabiliwa na hatari kubwa.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Nov 08, 2018 03:12 UTC
  • Amnesty: Maisha ya raia wa al Hudaidah, Yemen yamo hatarini

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mapigano makali yanayoendelea katika mkoa wa al Hudaidah huko kwenye pwani ya magharibi mwa Yemen na kusema kuwa, maisha ya raia katika eneo hilo yanakabiliwa na hatari kubwa.

Taarifa ya Amnesty International imesema kuwa, raia wa Yemen katika mkoa wa al Hudaidah ndio wanaolipa gharama kubwa kutokana na mapigano makali yanayoendelea katika eneo hilo baina ya mamluki wa Saudi Arabia na jeshi la Yemen likishirikiana na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah. 

Awali Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) lilikuwa limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya raia hususan watoto wadogo katika mkoa wa al Hudaidah na kusema kuwa, hata watoto wanaolazwa mahospitalini hawakusalimika na mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake.

Mji wa al Hudaidah una bandari ya kistratijia ambayo inahesabiwa kuwa njia muhimu na pekee ya misaada ya kibinadamu inayotumwa Yemen, na asilimia 70 ya misaada yote ya chakula, dawa na vifaa vya tiba vinaingizwa Yemen kupitia bandari hiyo ambayo sasa inazingirwa na Saudi Arabia.

Maelfu ya Wayemeni wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi makali yaliyoanzishwa na Saudi Arabia miaka mitatu iliyopita dhidi ya nchi hiyo ikisaidiwa na nchi kadhaa hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.