WFP: Mamilioni ya Wayemen watakufa njaa vita vikiendelea
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani, WFP, limetahadharisha kuwa iwapo vita havitamalizika Yemen, mamilioni ya Wayemen watakufa njaa.
WFP inataka mapigano ya sasa katika mji wa bandari wa Hodeidah yakomeshwe mara moja kwani mbali ya kuangamiza maisha ya watu yanaongeza idadi ya waathirika wa njaa linalowapa msaada wa chakula, iliyopanda kutoka milioni 8 hadi milioni 14.
Bandari ya Hodeidah ambayo ndiyo uti wa mgongo wa Yemen hutumika kuingizia chakula na mafuta ukizingatia kwamba asilimia 90 ya chakula cha Yemen kinatoka nje. Hata hivyo vikosi vamizi vinavyoongozwa na Saudia vimekuwa vikitekeleza mashambulizi dhidi ya bandari hiyo ya kistratijia kwa lengo la kuidhibiti.
Wito huo wa WFP umejiri baada ya asasi 35 za kimataifa zisizo za kiserikali kutaka kukomeshwa mara moja mashambulizi ya kikatili yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi maskini wa nchi ya Kiarabu na Kiislamu ya Yemen.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.