Bin Salman baina ya wahka wa ndani na malalamiko ya kimataifa
Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman yuko katika safari ya kuzitembelea nchi 6 za Kiarabu na inatazamiwa kuwa, baada ya safari hiyo ataelekea Argentina kushiki mkutano wa G20. Hata hivyo Bin Salman amepatwa na wahka na wasiwasi mkubwa kutokana na uwezekano wa kutokea mapinduzi ndani ya kizazi cha Aal Saud na malalamiko yanayozidi nje ya nchi hiyo.
Mrithi huyo wa Kiti cha Ufalme wa Saudia anazitembelea nchi za Imarati, Bahrain, Tunisia, Algeria, Mauritania na Misri. Safari hiyo imeathiriwa na hatua za Bin Salman na jinai zake kubwa ikiwa ni pamoja na mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utaweala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi na kushindwa utawala wa Riyadh katika vita vyake dhidi ya watu wa Yemen. Ndani ya nchi pia Bin Salman anakabiliwa na mashinikizo makubwa ya wanamfalme wenzake katika ukoo wa Aal Saud na vilevile mashinikizo ya walimwengu nje ya nchi hiyo.
Mkosoaji na mfichuaji wa habari za ndani ya utawala wa Saudi Arabia, maarufu kwa jina la Mujtahid amefichua kwamba, ofisi ya mfalme wa Saudia imechanganyikiwa na kwamba idadi kubwa ya maafisa ambao walipangwa kufuatana na Bin Salman katika safari ya kuelekea Argentina kwenye mkutano wa G20 wamefuta safari zao na kurejea Saudia. Baadhi ya maafisa hao wameitwa ofisi ya mfalme nyakati za usiku na kunashuhudiwa harakati kubwa za kiusalama karibu na ofisi hiyo. Mujtahid pia ameuambia mtandao wa Khaleej Online kwamba: "Bin Salman ameamuru kuchukuliwa hatua za dharura za usalama na amekitaka kikosi maalumu cha Gadi ya Mfalme wa Saudia kuondoka katika maeneo ya mashariki na magharibi mwa nchi na kuelekea Riyadh ili kuzuia jaribio lolote la mapinduzi."
Huko nje ya nchi pia Muhammad bin Salman anaendelea kuandwamwa na mashinikizo na malalamiko makubwa ya walimwengu. Katika nchi za Tunisia, Algeria na Mauritania wananchi wanaendelea kumwandika Bin Salman katika mitandao ya kijamii na kumwita "mrithi wa ufalme mwenye msumeno", wakiashiria jinsi maafisa wa utawala wa Saudi Arabia walivyomuua kigaidi Jamal Khashoggi na baadaye wakamtaka vipande vipande kwa amri ya Bin Salman.
Waandamanaji na wapinzani wa safari ya Bin Salman katika nchi hizo wanaamini kuwa mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia anafanya jitihada za kufuta ukurasa mchafu wa sera zake chafu ikiwa ni pamoja na mauaji ya mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Riyadh, Jamal Khashoggi na jinai zinazoendelea kufanywa na Saudia huko Yemen.
Malalamiko na upinzani wa safari ya Bin Salman katika nchi kadhaa za Kiarabu hayakuishia kwa raia wakaida. Imed Daïm ambaye ni mjumbe wa Harakati ya Irada ya Tunisia na mwanachama wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la nchi hiyo amesema: Bin Salman katili na muuaji hana nafasi yoyote nchini kwetu."
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Amani ya Algeria Abdul Razaq Muqri amesema: Bin Salman ni katili na muuaji wa watoto wa Yemen na anaendelea kuwasweka jela wasomi na wanafikra wengi wa Saudia na hakaribishwi hapa Algeria."
Inatazamiwa kuwa safari ya Muhammad bin Salman nchini Argentina itaandamana na matatizo mengi na wasimamizi wa mkutano wa G20 wana wasiwasi kwamba, kuwepo kwa mrithi huyo wa kiti cha Ufalme was Saudia mjini Buenos Aires kusababisha machafuko na huenda mashambulizi ya kigaidi. Gazeti la The Guardian la Uingereza limeandika kuwa: Viongozi wanaotarajwia kushiriki kutano wa G20 nchini Argentina wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na ushiriki wa Bin Salman katika mkutano huo.
Hali inayomkabili Bin Salman ndani na nje ya Saudi Arabia inamwandama pia bwana wake, yaani Donald Trump kwa njia moja au nyingine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Rais huyo wa Marekani amefumbia jicho jinai na mauaji yanayofanywa na Bin Salman kwa tamaa ya fedha na dola za mafuta za Saudi Arabia na anaendelea kumkingia kifua mbele ya hasira za walimwengu. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, hiyama ya Trump haitaweza kumuondoa Bin Salman katika shimo na kinamasi cha sasa.