Syria yakataa mpango wa kuundwa serikali ya mpito
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Miqdad amesema serikali ya Damascus inapinga pendekezo la wapinzani la kuundwa serikali ya mpito nchini humo.
Faisal al-Miqdad amefafanua kuwa pendekezo la wapinzani wa serikali ya Syria la kuundwa serikali ya mpito maana yake hasa ni kutaka kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad, na ni sawa na kufanya mapinduzi, na kwamba wananchi wa Syria hawatoruhusu kutekelezwa mpango kama huo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya mgogoro wa nchi hiyo Rais Assad amekuwa katika vita vya kupambana na magaidi na kwamba ni Uturuki na Saudi Arabia tu ndizo zinazong'ang'ania kiongozi huyo ang'atuke madarakani ili kudhamini maslahi yao.
Kuhusiana na utatuzi wa mgogoro wa Syria, Al-Miqdad amesisitiza kuwa ili kuweza kupiga hatua katika mchakato wa utatuzi wa mgogoro huo inapasa zichukuliwe hatua za dhati na za kivitendo; na jambo hilo linaweza kufikiwa kwa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa au serikali pana zaidi itakayojumuisha pia wawakilishi wa upinzani.
Kuhusu sababu ya kuendelea kwa muda mrefu mazungumzo na wapinzani wa serikali bila ya kupatikana tija, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwepo hitilafu baina ya wapinzani kumekwamisha kupatikana makubaliano thabiti katika mazungumzo hayo.../