Kukiri Marekani kushindwa siasa zake za kuipindua serikali ya Syria
Mgogoro wa Syria na vita vya ndani vya nchi hiyo vilivyoanza mwaka 2011 vimeitumbukiza nchi hiyo ya Kiarabu katika mgogoro mkubwa. Suala hilo linatumiwa vibaya pia na madola ya kibeberu ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kwa kushirikiana na vibaraka wake wa nchi za Kiarabu kama vile Saudi Arabia kumalizia hasira zao kwa taifa hilo.
Lakini licha ya njama kubwa za muungano wa Magharibi-Kiarabu za kuyasaidia kwa kila hali magenge ya wakufurishaji yaliyokuwa yamekula kiapo cha kuiangusha serikali ya Rais Bashar al Assad iliyoko madarakani kihalali huko Syria, hivi sasa madola ya Magharibi hasa Marekani yamelazimika kukiri kuwa yamefeli katika siasa zao za kutaka kuipindua serikali ya Damascus. Uwepo wenye athari nzuri wa Iran na harakati ya Hizbullah ya Lebanon huko Syria na hatua ya Russia ya kuisaidia kijeshi Syria tangu mwezi Septemba 2015 ni miongoni mwa mambo ambayo yameliletea taifa hilo la Kiarabu ushindi mkubwa.
Marekani ambayo ni dola la kibeberu la Magharibi linalojali tu maslahi yake kwa kushirikiana na mabeberu wengine wa Ulaya kama vile Uingereza na Ufaransa, tangu mwaka 2011 yanaendesha njama zao huko Syra lengo lao kuu likiwa ni kujaribu kuivunja nguvu kambi ya muqawama na kuipindua serikali inayotawala kisheria nchini Syria. Madola hayo ya kibeberu hayajawahi kusimamisha hata mara moja uungaji mkono wao kwa magenge ya kigaidi ambayo yalikuwa na ndoto kuwa yangeliweza kuipindua serikali ya Rais Bashar al Assad.

Kwa kweli Washington na waitifaki wake nchi za Ulaya na za Kiarabu zimelazimika kubadilisha stratijia zao na kwamba njama inayoendeshwa na maadui hao wa taifa la Syria hivi sasa ni kutaka kuiweka madarakani serikali inayounga mkono Magharibi kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo ubunifu uliofanywa na Iran, Uturuki na Russia katika uwanja huo umefelisha njama hizo za Magharibi. Nchi hizo tatu zinaongoza juhudi za kuutafutia suluhisho la kisiasa mgogoro wa Syria na zimefanikiwa sana katika juhudi zao hizo.
Tab'an mafanikio hayo ya nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki hayawezi kuwafurahisha mabeberu wa Magharibi hasa Marekani ambayo ndiyo iliyo na nafasi kubwa ya kuendelea mgogoro na vita ndani ya Syria kutokana na uungaji mkono wake wa wazi kwa magenge ya kigaidi.
James Jeffrey, mwakilishi maalumu wa Marekani katika kadhia ya Syria amekiri kuwa, Washington haina nia tena ya kuipindua serikali ya Syria. Akizungumza katika kikao cha kituo cha utafiti cha Baraza la Atlantiki mjini Washington, Jeffrey amesema: Tunachotaka sisi ni kuweko utawala wenye siasa nyingine huko Syria na hiyo haina maana ya kuipindua serikali iliyopo madarakani hivi sasa. Sisi hatufanyi juhudi za kumpindua Bashar al Assad.

Kwa kweli matamshi hayo ya mjumbe wa Marekani katika masuala ya Syria ni uthibitisho wa kushindwa njama za Marekani za kutaka kuipindua serikali ya Damascus.
Hata hivyo, hiyo haina maana ya kumalizika uadui wa Marekani kwa taifa la Syria. Na ndio maana rais wa Marekani, Donald Trump akasema wazi kuwa Washington itashiriki katika ujenzi mpya wa Syria kama tu serikali ya nchi hiyo itabadilisha siasa zake na kukubali kuwa chini ya Magharibi. Kwa maneno mengine ni kwamba inachotaka Marekani ni serikali ya Rais Bashar al Assad ijitoe katika kambi ya muqawama na ikubali kuburuzwa na madola ya Magharibi.
Hilo linaonekana wazi katika matamshi ya James Jeffrey, mwakilishi wa Marekani katika suala la Syria. Amesema: Nchi za Magharibi zina hamu kubwa ya kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuijenga upya Syria, lakini jambo hilo halitotendeka hadi pale serikali ya Damascus iachane na siasa zake za hivi sasa ili kuzuia nchi hiyo isije ikakumbwa na mgogoro mwingine kama huo. Vile vile amesema, Marekani inakubali Iran kuwa na nafasi yake ya kidiplomasia huko Syria.
Kuiingiza Iran katika mjadala huo kunaonesha namna Wamarekani wanavyochukizwa na juhudi za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutatua migogoro ya eneo hili. Ukweli wa mambo ni kuwa Iran iko Syria kwa ombi rasmi la serikali inayotawala kisheria nchini humo. Iran inatoa mchango wa kuishauri serikali ya Damascus katika vita vyake dhidi ya ugaidi na kwa hakika imepata mafanikio makubwa katika suala hilo. Ni wazi kuwa, jambo hilo haliwezi kuifurahisha hata chembe Marekani na mabeberu wengine.