Jordan yaitaka Israel iondoke kwenye Miinuko ya Golan ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50753-jordan_yaitaka_israel_iondoke_kwenye_miinuko_ya_golan_ya_syria
Jordan imeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uheshimu sheria za kimataifa na uondoke haraka iwezekanavyo katika Miinuko ya Golan ya Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2019 13:29 UTC
  • Jordan yaitaka Israel iondoke kwenye Miinuko ya Golan ya Syria

Jordan imeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uheshimu sheria za kimataifa na uondoke haraka iwezekanavyo katika Miinuko ya Golan ya Syria.

Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ametoa mwito huo mjini Amman katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo na kuongeza kuwa, "Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu ni milki ya Syria. Sheria ya kimataifa iko wazi kuhusiana na jambo hilo, na kwa msingi huo Tel Aviv inapaswa kuondoa vikosi vyake katika eneo hilo."

Safadi ameongeza kuwa, Israel inapaswa kuondoka mara moja katika eneo hilo unaolikalia kwa mabavu la Syria, katika fremu ya makubaliano ya amani na kwa misingi ya sheria ya kimataifa.

Bendera ya Syria katika Miinuko ya Golan

Uhusiano wa utawala pandikizi wa Israel na Jordan umeonekana kuzidi kuharibika katika miezi ya hivi karibuni. Siku chache zilizopita, Abdul Nasser Abul Bassal, Waziri wa Waqfu wa Jordan alitahadharisha kuhusiana na kuendelea uvamizi na hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa, qibla cha kwanza cha Waislamu, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Aidha mwishoni mwa mwaka uliomalizika, Kamisheni ya Palestina katika Bunge la Jordan ilisema kuna haja ya bendera ya Israel kuwekwa chini katika milango ya majengo na idara zote za serikali ili watu wote wanaoingia katika idara hizo waikanyage bendera hiyo ya utawala huo haramu.