Jan 21, 2019 01:32 UTC
  • Mwaka 2019, mwaka mbaya zaidi kwa haki za binaadamu nchini Bahrain

Kamati ya watu waliotiwa mbaroni katika Ukanda wa Pwani nchini Bahrain imetangaza kwamba, katika jela ya Jau nchini Bahrain, maafisa usalama wa utawala wa Aal-Khalifa na katika kulipiza kisasi dhidi ya wafungwa wa kesi za uhuru wa kujieleza, wanatekeleza siasa za kuwatesa kwa njaa wafungwa hao.

Kwa mujibu wa duru za habari, kupitia siasa hizo zilizo dhidi ya binaadamu, wanaharakati kadhaa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika korokoro za utawala huo, sasa wanakabiliwa na kifo cha taratibu. Tangu kulipoanza mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011, viongozi wa utawala wa Aal-Khalifa walitangaza wazi wazi kutekeleza siasa za ukandamizaji na ukatili kwa ajili ya kuwafanya wanamapinduzi na wanaharakati wa kisiasa, wasalimu amri. Kwa mujibu wa Jalal Firuz, mwakilishi wa zamani katika bunge la Bahrain ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya kisheria nchini humo, hadi sasa serikali ya Manama inawashikilia zaidi ya wafungwa wa kisiasa 5000 na kwa mujibu wa takwimu, nchi hiyo ndiyo inashika nafasi ya kwanza kati ya nchi za dunia zenye wanasiasa wengi wanaozuiliwa korokoroni.

Sehemu ya ukandamizaji wa utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa katika kuvamia makazi ya raia

Katika mazingira hayo, anga ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa Bahrain bado inaendelea kushuhudiwa ambapo mwaka uliopita wa 2018 wapinzani wa serikali walikuwa na wakati mgumu zaidi kutokana na ukandamizaji kama vile wa kuwafunga jela kupitia hukumu za kidhalimu, miamala mibaya na kuwavua uraia wapinzani hao. Aidha mwaka uliopita makumi ya raia wa Bahrain walivuliwa uraia na utawala wa kidekteta wa Aal-Khalifa na kwa mujibu wa takwimu, idadi ya watu waliovuliwa uraia katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni nchini humo imefikia 810. Mbali na hayo ni kwamba wapinzani 14 wa nchi hiyo pia wanasubiria kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi yao wakiwa jela. Kamatakamata iliyopindukia dhidi ya wanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain na kadhalika kutolewa hukumu kali dhidi yao, ikiwemo hukumu ya kifo, ni mambo yayokinzana na kipengee cha 10 cha hati ya kimataifa ya haki za binaadamu na kadhalika kipengee cha 6 cha mkataba maalumu wa haki ya uraia na kisiasa. Aidha katika suala la kuvuliwa uraia, kipengee cha 15 cha azimio la la kimataifa la haki za binaadamu kinaeleza kwa uwazi kwamba: "Watu wote wanayo haki ya kustafidi na uraia wao na hakuna mtu aliye na haki ya kujichukulia sheria mkononi na kumnyima uraia mtu mwingine." Ama nukta inayofaa kuashiriwa hapa ni kwamba, ripoti mpya iliyotolewa kuhusiana na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu nchini Bahrain inatabiri kuwa hali ya mambo nchini Bahrain katika mwaka huu wa 2019 itakuwa mbaya zaidi.

Sheikh Ali Salman, kiongozi wa vuguvugu la wananchi ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka mingi jela kwa tuhuma bandia

Hii ni kwa kuwa miamala ya ukandamizaji na ukatili wa utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wapinzani imeibua wasi wasi mkubwa duniani, na hasa miongoni mwa taasisi za haki za binaadamu kuhusiana na hali na hatma ya wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa utawala wa Aal-Khalifa. Hatua za utawala huo pamoja na mambo mengine, zimeweka wazi utambulisho halisi wa kidikteta wa utawala huo ambao hautambui lolote ispokuwa ukandamizaji na ukatili kama ambavyo haufungamani na sheria wala mikataba yoyote ile. Kwa hakika siasa za ukandamizaji za utawala huo hazijakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuongeza idadi ya wafungwa wa kisiasa wa utawala huo. Ukweli ni kwamba, utawala huo katika kuwafuatilia wanaharakati wa kisiasa ambao wanapigania utawala wa sheria nchini , unatumia tuhuma zisizo na msingi na kadhalika hatua nyingine za kidhalimu dhidi ya wanaharakati hao. Kwa hatua hizo, utawala wa Aal-Khalifa unaibua khofu na hali ya woga kati ya wanaharakati wa kisiasa nchini humo ili kwa njia hiyo uweze kuhitimisha malalamiko ya wananchi yaliyoanza mwaka 2011. Ni kwa kuzingatia hilo, ndipo ukatekeleza hatua za ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu ikiwemo kamatakamata ya kidhalimu, mashambulizi dhidi ya makazi ya raia, vifungo visivyo vya uadilifu, ukandamizaji wa maandamano ya amani na pia kuwanyang'anya wapinzani uraia wao. Matokeo ya siasa za watawala wa Bahrain ni kushadidi anga ya ukatili na upolisi nchini humo tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2019, hali ambayo imetolewa tahadhari na asasi za kisheria.

Tags