Kufichuliwa misaada mipya ya madola ya Magharibi kwa magaidi wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51059-kufichuliwa_misaada_mipya_ya_madola_ya_magharibi_kwa_magaidi_wa_syria
Valery Shkolnik, Msemaji wa Majeshi ya Russia nchini Syria ametangaza habari ya kugunduliwa ghala moja kubwa la silaha za magenge ya kigaidi katika mji wa Darayya huko Syria, ambapo sehemu kubwa ya silaha hizo zimetoka Marekani na nchi za Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2019 02:42 UTC
  • Kufichuliwa misaada mipya ya madola ya Magharibi kwa magaidi wa Syria

Valery Shkolnik, Msemaji wa Majeshi ya Russia nchini Syria ametangaza habari ya kugunduliwa ghala moja kubwa la silaha za magenge ya kigaidi katika mji wa Darayya huko Syria, ambapo sehemu kubwa ya silaha hizo zimetoka Marekani na nchi za Ulaya.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel nao umeshadidisha chokochoko zake za kufanya mashambulizi ya kulenga na kukimbia huko Syria kwa baraka kamili za Marekani, lengo likiwa ni kuhakikisha magenge ya kigaidi hayavunjiki moyo bali yanaendelea na jinai zao katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kuna masuala kama vile kuongezeka mashambilizi ya utawala wa Kizayuni nchini Syria na kupanda zaidi kiwango cha misaaada ya Marekani na watawala vibaraka wa nchi za Kiarabu kwa magenge ya kigaidi, yote hayo ni katika juhudi za waungaji mkono wa magaidi hao za kuhakikisha kuwa mamluki wao watenda jinai hawakati roho kikamilifu nchini Syria. Ukweli wa mambo ni kwamba hali inavyoendelea Syria hivi sasa inaonesha kuwa nchi hiyo imeshaingia kivitendo katika kipindi kipya cha harakati na mashambulizi ya mihimili ya shari yaani utawala wa Kizayuni waIisrael na magenge ya kigaidi, makundi mawili ambayo kwa namna moja au nyingine yanaungwa mkono na Magharibi. Tunapoitupia jicho na kuichanganua hali ya Syria hivi sasa tutaona kwamba kuna njama kubwa zilizoelekezwa kwa nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu ambayo iko katika eneo muhimu sana la kiistratijia na ni moja ya nguzo kuu za kambi ya muqawama kwenye eneo hili. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Magharibi zilianzisha uvamizi wao katika eneo hili kwa madai ya kupambana na ugaidi. Nchi hizo za kibeberu zinazigonganisha vichwa nchi za eneo hili, lengo lao kuu likiwa ni kuendeleza fitna zao za kikoloni na kiistikbari. Ni kwa sababu hiyo ndio maana tunaona jinsi ushirikiano baina ya magenge ya kigaidi na madola ya Magharibi unavyozidi kuongeza jinai dhidi ya wananchi wasio na hatia hasa huko huko Syria na Yemen.

Baadhi ya silaha zilizokamatwa na jeshi la Syria kutoka kwa magaidi

 

Gazeti la The Guardian la nchini Uingereza limesambaza ripoti kuhusu suala hilo na kuandika kwamba katika mazungumzo waliyofanyiwa viongozi wa Marekani Uingereza, viongozi hao wamezungumzia machaguo tofauti waliyo nayo kuhusiana na Syria kama vile kuyapelekea magenge ya kigaidi misaada ya kijeshi kwa kutumia myavuli maalumu. Hii ni katika hali ambayo kituo cha utafiti cha Carter cha nchini Marekani nacho kimefichua waziwazi kuwa, genge la kigaidi la Jabhatun Nusra na magenge mengine 23 ya kigaidi yametumiwa misaada ya kijeshi mara nyingi sana na Marekani. Gazeti la Wall Street Journal la nchini Marekani nalo hivi majuzi liliandika kuwa, katika miaka ya hivi karibu, Israel imeyapa misaada ya aina mbalimbali magenge tofauti ya kigaidi huko Syria kama vile silaha, fedha na mishahara ya kila mwezi kwa kutumia kikosi maalumu kilichoanzishwa na utawala huo pandikizi wa Israel kuendesha njama hiyo. 

Kusema kweli harakati ya kishujaa ya jeshi la Syria iliyolenga kuwamaliza na kuwasafisha kikamilifu magaidi nchini humo imewatia hofu sana waungaji mkono wa magaidi hao hasa Marekani na utawala wa Kizayuni. Hofu hiyo imeyafanya madola ya kibeberu kama vile Marekani kuamua kudhihirisha wazi zaidi uungaji mkono na misaada yao hasa ya kijeshi kwa magenge ya kigaidi nchini Syria. Pamoja na hayo, njama za madola ya kibeberu kama vile Marekani, Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni pamoja na vibaraka wao viongozi wa baadhi ya nchi za Kiarabu zimeshindwa huko Syria. Kufeli huko kumekuja licha ya madola hayo kufanya njama kubwa ya kuisambaratisha Syria na kuipindua serikali yake inayotawala kisheria nchini humo. Madola hayo yametumia fedha nyingi kufadhili magenge hatari ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS), Jabhatun Nusra, Ahrarush Sham n.k, lakimi yameshindwa. Hata hivyo na licha ya kufeli kote huko, lakini utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na mabeberu wengine na vibaraka wao wanaonekana bado wana ndoto ya kufikia malengo yao haramu nchini Syria kupitia kuongeza misaada yao kwa magaidi kwa sura na muundo mpya. Katika kipindi cha utawala wa rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump, mafunzo ya kijeshi na silaha za Marekani kwa magaidi wa Syria zimeongezeka na jambo hilo linazidi kudhihirisha uongo wa madai ya Marekani ya kuondoka kijeshi huko Syria. Weledi wa mambo wanasema, madai hayo ya Marekani si kitu kingine ila hila na njama nyingine tu za Washington dhidi ya taifa la Syria.

Shehena nyingine ya silaha za madola ya kibeberu walizoshehenezwa magaidi nchini Syria ili kufanya jinai dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali ya nchi hiyo.