Amnesty yaitaka Uingereza kusitisha uuzaji silaha kwa Saudia
Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Uingereza isitishe uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen.
Ripoti iliyotolewa na Amnesty International kabla ya safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Jeremy Hunt katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi imekumbusha mashambulizi yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya hospitali, shule, mabasi yanayobeba wanafunzi wa Yemen na kadhalika na kuitaka serikali ya London isitishe uuzaji silaha kwa Saudi Arabia na washirika wake hadi pale itakapopatikana amani nchini Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza hii leo anataamiwa kuanza safari ya kuzitembelea nchi za Saudi Arabia, Imarati na Oman.
Saudi Arabia ikiungwa mkono na kusaidiwa na Marekani, Imarati, Israel na washirika wao wengine na kwa kutumia silaha za nchi za Magharibi hususan Uingereza, ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo na mashambulizi hayo yamesababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vita dhidi ya Yemen.