UN yaiokosoa Israel kwa kupinga ripoti ya mauaji ya Wapalestina Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51990-un_yaiokosoa_israel_kwa_kupinga_ripoti_ya_mauaji_ya_wapalestina_gaza
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Israel kupinga ripoti ya wataalamu wa umoja huo kuhusu mauaji ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza yaliyofanywa na askari katili wa utawala huo haramu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 06, 2019 23:23 UTC
  • UN yaiokosoa Israel kwa kupinga ripoti ya mauaji ya Wapalestina Gaza

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Israel kupinga ripoti ya wataalamu wa umoja huo kuhusu mauaji ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza yaliyofanywa na askari katili wa utawala huo haramu.

Amesema inasikitisha kuiona Israel inapinga moja kwa moja ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa bila kuzungumzia masuala muhimu yaliyoakisiwa kwenye ripoti yenyewe.

Ripoti hiyo iliyotolewa wiki iliyopita na wataalamu wa UN inasema, ushahidi unaonesha kuwa utawala wa Israel ulifanya jinai dhidi ya binadamu wakati wa kukabiliana na maandamano ya amani ya mwaka 2018 ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Timu hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilikusanya ripoti za jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na walenga shabaha stadi na makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, Wapalestina 189 waliokuwa katika maandamano ya 'Haki ya Kurejea' waliuawa mwaka jana na wanajeshi wa Israel, huku wengine 6,100 wakijeruhiwa.

Majeruhi wa Kipalestina katika maandamano ya haki ya kurejea

Tangu tarehe 30 Machi mwaka jana Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wamekuwa wakifanya maandano yaliyopewa jina la Haki ya Kurejea katika kila siku za Ijumaa.

Tangu wakati huo jeshi la Israel limekuwa likishambulia maandamano hayo ya amani ambapo hadi sasa limeua shahidi raia wasiopungua 260 wa Palestina na kujeruhi wengine zaidi ya elfu 27.