Wairaq watangaza mshikamano na waathiriwa wa mafuriko nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52534
Kufuatia mafuriko yaliyoikumba mikoa kadhaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, makundi tofauti ya Wairaq yametangaza mshikamano wao na waathirika wa mafuriko hayo kwa kuchukua hatua ya kukusanya misaada ya fedha na isiyo ya fedha kwa ajili ya watu hao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 31, 2019 13:15 UTC
  • Wairaq watangaza mshikamano na waathiriwa wa mafuriko nchini Iran

Kufuatia mafuriko yaliyoikumba mikoa kadhaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, makundi tofauti ya Wairaq yametangaza mshikamano wao na waathirika wa mafuriko hayo kwa kuchukua hatua ya kukusanya misaada ya fedha na isiyo ya fedha kwa ajili ya watu hao.

Katika uwanja huo, Harakati ya Al-Nujaba ya Iraq imeanzisha kampeni ya nchi nzima iliyopewa jina la 'Wakati tuliposhambuliwa na magaidi mlitusaidia, sasa nanyi mmekumbwa na mafuriko, ni zamu yetu kukusaidieni.' Kufuatia kampeni hiyo makundi ya watu tofauti wa nchi hiyo wamekuwa wakiwasilisha misaada mbalimbali kwa ajili ya raia wa Iran waliokumbwa na mafuriko hayo katika ofisi za harakati hiyo mjini Baghdad, Basra, Najaf, Karbala, Al Diwaniyah, Diyala, Babil, Maysan, Muthanna Dhi Qar na Saladin.

Harakati ya Al-Nujaba ya Iraq ambayo imesimamia ukusanyaji wa misaada kwa ajili ya Wairan

Aidha katika kampeni hiyo Harakati ya Al-Nujaba ya Iraq imeashiria umuhimu wa uungaji mkono wa wananchi kwamba, hii ni fursa ya kipekee kwa ajili ya kutoa jibu la msaada uliowahi kutolewa na wananchi wa Iran katika kipindi ambacho Iraq ilikuwa chini ya mashambulizi ya kila upande ya magaidi wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS). Kufuatia mvua za hivi karibuni katika mikoa kadhaa ya Iran ikiwemo Golestan, Mazandaran, Fars, Lorestan na Kermanshah wakazi wa mikoa hiyo walikumbwa na mafuriko makubwa. Katika tukio hilo kwa akali watu 45 wamepoteza maisha na mamia ya wengine wamejeruhiwa sambamba na kusababishwa hasara kubwa ya kimaada. Itakumbukwa kuwa baada ya kundi la ukufurishaji na kigaidi la Daesh (ISIS) linaloungwa mkono na Marekani, Israel, Saudia n.k kuvamia nchi ya Iraq na kudhibiti miji mingi ya nchi hiyo ya Kiarabu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa mstari wa mbele kwenda kuwasaidia Wairaq kulitokomeza genge hilo lenye kufuata idolojia ya Uwahabi ambalo lilikuwa likitekeleza jinai kubwa dhidi ya Waislamu wa Shia na Suni na hata watu wasio Waislamu pia.