Wabunge wa Bahrain wakosoa kualikwa Wazayuni katika Kongamano la Biashara
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52555-wabunge_wa_bahrain_wakosoa_kualikwa_wazayuni_katika_kongamano_la_biashara
Wabunge wa Bahrain wamekosoa vikali hatua ya kualikwa wazungumzaji kadhaa wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Kongamano la Kibiashara linalotazamiwa kufanyika katika kipindi cha wiki mbili zijazo nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 01, 2019 10:32 UTC
  • Wabunge wa Bahrain wakosoa kualikwa Wazayuni katika Kongamano la Biashara

Wabunge wa Bahrain wamekosoa vikali hatua ya kualikwa wazungumzaji kadhaa wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Kongamano la Kibiashara linalotazamiwa kufanyika katika kipindi cha wiki mbili zijazo nchini humo.

Wabunge wa Bahrain wametoa taarifa ya pamoja inayopinga kukaribishwa nchini humo viongozi hao wa Kizayuni. Taarifa hiyo imebainisha kuwa, "Bunge linasisitizia uungaji mkono wake kwa kadhia ya wananchi wa Palestina, na hilo litasalia kuwa kipaumbele kwa Wabahrain na Waarabu wote."

Bahrain kama aghalabu ya nchi za Kiarabu haina uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel. Waisraeli wanne ni miongoni mwa makumi ya watu walioalikwa kuzungumza katika mkutano huo wa wawekezaji unaotazamiwa kufanyika mjini Manama kati ya Aprili 15 na 18.

Hii ni katika hali ambayo, gazeti la Al-Quds Al-Arabi limemnukuu Abdullah Al-Kandari, mwakilishi wa bunge nchini Kuwait akisema kuwa, Waziri wa Viwanda wa nchi hiyo, Khaled Al-Rawdan amelazimika kususia mkutano huo wa kibiashara nchini Bahrain, kutokana na ushiriki wa idadi kadhaa ya viongozi wa Kizayuni katika mkutano huo uliopewa jina la 'Ujasiriamali'.

Saudia, Imarati na Misri ni miongoni mwa nchi za KIarabu zinazotaka kufanywa wa kawaida uhusiano na Israel

Aidha wabunge wa Kuwait wamezitaka nchi nyingine kususia kongamano hilo la mjini Manama na wametangaza kwamba ushiriki wake una maana ya kuboresha uhusiano na utawala khabithi wa Kizayuni unaoukalia kwa mabavu mji wa Quds, kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu duniani.

Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya watawala wa Kiarabu wamekuwa wakifanya juu chini kuboresha mahusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.