Wazayuni washiriki kinyemela mkutano wa biashara nchini Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52932-wazayuni_washiriki_kinyemela_mkutano_wa_biashara_nchini_bahrain
Imebainika kuwa, ujumbe wa kibiashara na kisiasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshiriki kwa siri kubwa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama nchini Bahrain licha ya waandalizi wa mkutano huo kudai kuwa Wazayuni hao hawataushiriki kutokana na sababu za kiusalama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 18, 2019 09:12 UTC
  • Wazayuni washiriki kinyemela mkutano wa biashara nchini Bahrain

Imebainika kuwa, ujumbe wa kibiashara na kisiasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshiriki kwa siri kubwa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama nchini Bahrain licha ya waandalizi wa mkutano huo kudai kuwa Wazayuni hao hawataushiriki kutokana na sababu za kiusalama.

Afisa wa ngazi za juu wa utawala haramu wa Israel ambaye hakutaka kutaja jina lake amenukuliwa na kanali ya 13 ya utawala huo khabithi akisema kuwa, ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel umeshiriki kongamano hilo la kibiashara mjini Manama, sambamba na kufanya vikao vya pambizoni mwa mkutano huo na viongozi wa Bahrain.

Awali duru mbalimbali za nchini Bahrain zilikuwa zimetangaza kuwa, Wazayuni 45 wakiongozwa na Eli Cohen, Waziri wa Uchumi wa utawala wa Kizayuni walipanga kushiriki mkutano huo wa kimataifa ulioanza Jumatatu tarehe 15 Aprili na kumalizika leo tarehe 18.

Hata hivyo siku chache baadaye shirika la habari la Reuters lilimnukuu Jonathan Ortmans, mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama akisema kuwa, ijapokuwa utawala wa Bahrain uliushauri ujumbe huo wa Israel kushiriki katika mkutano huo, lakini Wazayuni hao waliamua kutoshiriki mkutano huo wakidai kuwa masuala ya kiusalama ndiyo yaliyowafanya wachukue uamuzi huo.

Wabahrain wakipinga Israel kushiriki mkutano wa FIFA  mwaka 2017

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua ya ujumbe huo wa Israel ya kuvunja safari yake nchini Bahrain imechukuliwa baada ya bunge la nchi hiyo kulaani kualikwa Wazayuni katika mkutano huo sambamba na wananchi katika mitandao ya kijamii kupinga safari hiyo ya Wazayuni nchini mwao.

Wabunge wa Bahrain walitoa taarifa ya pamoja inayopinga kukaribishwa nchini humo viongozi hao wa Kizayuni. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, "Bunge linasisitizia uungaji mkono wake kwa kadhia ya wananchi wa Palestina, na hilo litasalia kuwa kipaumbele kwa Wabahrain na Waarabu wote."