Miqdad: Tutaikomboa miiinuko ya Golan kwa gharama yoyote
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwa kwa gharama yoyote ile Syria itaikomboa miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Faisal Miqdad ameyasema hayo alipokuwa akijibu matamshi ya jana ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kikao cha kila wiki cha baraza la mawaziri wa utawala huo kilichofanyika katika miinuko hiyo ya Golan ambapo alidai kuwa, Tel Aviv haina mpango wa kuondoka katika miiinuko ya Golan milele.
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kuwa ameitisha kikao hicho kwa makusudi katika miinuko ya Golan ili kuutangazia ulimwengu mzima kuwa Israel haitaliacha eneo hilo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema miinuko ya Golan ni milki ya Syria kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kwamba eneo hilo ambalo ni mali ya wananchi wa Syria litarejeshwa kutoka mikononi mwa Wazayuni. Faisal Miqdad amesema machaguo yote yapo mezani kwa ajili ya kuikomboa miiinuko ya Golan iliyoghusubiwa na Israel.