May 17, 2019 02:30 UTC
  • UNICEF: Watoto 7,300 wameuawa nchini Yemen tokea 2015

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema watoto wapatao 7,300 wameuawa nchini Yemen katika vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake tokea mwaka 2015 hadi sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore aliyasema hayo katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kufafanua kuwa, katika kila saa 24 nchini Yemen, mtoto mmoja ima huuawa, kujeruhiwa au kuingizwa vitani kwa nguvu.

Fore ameongeza kuwa, katika kila dakika 10, mtoto mmoja nchini Yemen anafariki dunia kutokana na magonjwa au sababu zinazoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa afisa huyo wa ngazi za juu wa UNICEF, watoto zaidi ya milioni 2 wamekatiziwa masomo yao kutokana na mapigano hayo, na kwamba moja kati ya kila shule tano nchini humo zimeharibiwa na mashambulio hususan ya anga yanayofanywa kila uchao.

Mabaki ya basi la shule lililoshambuliwa na ndge za kivita za Saudia nchini Yemen

UNICEF imezitaka pande zote na jamii ya kimataifa kufanya jitihada za kuzuia maafa ya baa la njaa nchini Yemen na kukidhi mahitaji ya raia wanaoteseka wa nchi hiyo. 

Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani na washirika wao dhidi ya watu wa Yemen tokea Machi mwaka 2015 yameua maelfu ya raia wasio na hatia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. 

Tags