UNICEF: Machafuko na njaa vinatishia maisha ya maelfu ya watoto wa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124486
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, ghasia na njaa vinatishia maisha ya watoto wa Sudan hususan katika mzozo wa jimbo la Darfur Kaskazini.
(last modified 2025-03-29T03:11:11+00:00 )
Mar 29, 2025 03:11 UTC
  • UNICEF: Machafuko na njaa vinatishia maisha ya maelfu ya watoto wa Sudan

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, ghasia na njaa vinatishia maisha ya watoto wa Sudan hususan katika mzozo wa jimbo la Darfur Kaskazini.

Taarifa iliyotolewa na UNICEF imetangaza kuwa machafuko na njaa vinatishia maisha ya watoto wasiopungua 825,000 wa Sudan katika mzozo wa jimbo la Darfur Kaskazini.

"Hatupaswi kufumbia macho Jahanamu inayoshuhudiwa sasa huko Sudan," amesema Sheldon Yett, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, akitoa wito wa kusitishwa mzozo nchini humo.

Akieleza kuwa zaidi ya watoto 70 wameuawa au kulemazwa mwaka huu pekee, Sheldon Yett ameongeza kuwa: "Takriban watoto 825,000 wamekumbwa na majanga yanayoongezeka karibu na El Fasher. Idadi hii inajumuisha kesi zilizothibitishwa tu, na kuna uwezekano kwamba idadi ya watoto hawa ni kubwa zaidi."

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilianza Aprili 2023 baada ya kushadidi mvutano wa kuwania madaraka kati ya majenerali wawili wa nchi hiyo, Mohammed Hamdan Dagalo, na Abdel Fattah al Burhan.