Qatar: Amani ya Palestina sharti ijumuishe suluhu inayokubaliwa na Wapalestina
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar sambamba na kukosoa mpango wa kufanyika mkutano wa Marekani wa kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain, imesema matakwa ya wananchi wa Palestina lazima yajumuishe kwenye mipango yoyote ya amani na maendeleo inayowahusu.
Taarifa ya wizara hiyo imesema, "Maendeleo ya kiuchumi yanayohitajika kwa ajili ya amani ya Palestina hayawezi kupatikana pasi na kujumuisha suluhu ya kisiasa, yenye uadilifu na inayokubaliwa na Wapalestina wenyewe."
Serikali ya Doha imebainisha kuwa, ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo, lazima kuweko na muamana, irada ya kisiasa na jitihada za pamoja za wadau wa kieneo na kimataifa.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imeongeza kuwa, suluhisho lenye haki na usawa ndio msingi wa kufikia mikakati yoyote ile ya maendeleo kwa ajili ya amani ya Palestina.
Mpango wa 'Muamala wa Karne' utazinduliwa na Marekani nchini Bahrain katika 'Kongamano la Kiuchumi' litakalofanyika mjini Manama Juni 25 na 26.
Wapalestina wamewataka Waislamu kote duniani kusimama kidete dhidi ya njama hizo batili za Marekani zilizopewa anwani ya "Muamala wa Karne".