Ansarullah: Mkutano wa Bahrain ni sehemu ya Saudia kuitumikia Israel
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, mkutano wa Marekani unaotazamiwa kufanyika nchini Bahrain mwishoni mwa mwezi huu wa Juni ni sehemu ya kujidhalilisha na kujipendekeza utawala wa Aal-Saud wa Saudia Arabia kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Abdul-Malik Badruddin al-Houthi alisema hayo katika taarifa ya jana Ijumaa na kubainisha kuwa, haiwezekani kufanya uhusiano na adui Mzayuni na kwamba kufanya uhusiano na utawala huo ni kupuuza kadhia muhimu ya Umma wa Kiislamu ambayo ni kadhia ya Palestina.
Amesema kikao hicho cha Manama ni sehemu ya mikakati mipana ya baadhi ya nchi vibaraka za Kiarabu zikiongozwa na Saudia, katika kutumikia maslahi ya utawala haramu wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoadhimishwa jana Ijumaa katika sehemu mbalimbali za dunia, Mkuu wa harakakati ya Ansarullah ya Yemen amesema, "Maandamano ya Siku ya Quds ni fursa ya kutathmini kadhia ya Palestina, na kuandaa hatua zinazotekelezeka kuhusu kadhia hiyo."
Marekani imetangaza kuwa itashirikiana na Bahrain kuwa mwenyeji wa kongamano litakalofanyika Juni 25-26 katika mji wa Manama kwa lengo eti la kuhimiza uwekezaji katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza ambao nao uko chini ya mzingiro.
Hata hivyo wananchi na viongozi wa Palestina wanasema lengo kuu la kongamano hilo ni kuandaa mazingira ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kuzindua kile ambacho kinatajwa kuwa ni 'Muamala wa Karne."
Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO), Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS zimetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kususia kongamano hilo ambalo Marekani imeitisha nchini Bahrain ambalo Wapalestina wanaamini kuwa linalenga kusambaratisha haki zao.