Idadi ya wahamiaji wa Kizayuni wanaokimbia kutoka Israel yaongezeka
Vyombo vya utawala haramu wa Kizayuni vimetangaza ongezeko la uhajiri wa walowezi wa Kizayuni kutoka ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Gazeti la utawala huo bandia la Haaretz limemnukuu Don Ben Devid, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi wa utawala wa Kizayuni kupitia ripoti iliyopewa jina 'Uhajiri Kinyume wa Walowezi wa Israel' ambapo amesema kwamba idadi ya raia wa Israel wanaokimbia kutoka radhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu imeutia wasi wasi mkubwa utawala huo. Kwa mujibu wa gazeti hilo, kuingia Mzayuni mmoja aliyeelimika ndani ya Israel, kunaenda sambamba na kuondoka Wazayuni wanne kutoka utawala huo (yaani Mzayuni mmoja, kwa Wazayuni wanne.) Hayo yanajiri katika hali ambayo kituo cha takwimu cha utawala wa Kizayuni Agosti 2017, sambamba na kuashiria taathira hasi ya changamoto za kijamii ndani ya Israel katika uga wa usalama, uchumi na jamii, kimesema kuwa uhajiri kinyume wa Wazayuni wanaokimbia Israel ni mara mbili zaidi ya idadi ya Wazayuni wanaoingia ardhi hizo za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel.)
Siasa za kupenda vita za utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi, kuwapa ahadi za uongo Mayahudi na kushindwa utawala huo kila mara mbele ya makundi ya muqawama wa Palestina, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa sababu ya walowezi wa Kizayuni kukimbia Israel kuelekea nchi nyingine za dunia.