Israel kushiriki mkutano wa Marekani dhidi ya Wapalestina, Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54171-israel_kushiriki_mkutano_wa_marekani_dhidi_ya_wapalestina_bahrain
Utawala wa Kizayuni wa Israel umethibitisha kuwa utashiriki mkutano wa 'kiuchumi wa Manama' nchini Bahrain ulioitishwa na Marekani, wenye lengo la kuzindua 'Muamala wa Karne'.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2019 03:16 UTC
  • Israel kushiriki mkutano wa Marekani dhidi ya Wapalestina, Bahrain

Utawala wa Kizayuni wa Israel umethibitisha kuwa utashiriki mkutano wa 'kiuchumi wa Manama' nchini Bahrain ulioitishwa na Marekani, wenye lengo la kuzindua 'Muamala wa Karne'.

Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala huo haramu, Yisrael Katz ameiambia kanali ya 13 ya televisheni ya Kizayuni mjini New York kuwa, Tel Aviv itatuma ujumbe kwenye mkutano huo. Baadhi ya duru za habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba, Israel itatuma ujumbe wa ngazi za juu kwenye mkutano huo, lakini hawatakuwa maafisa wa serikali.

Hii ni katika hali ambayo, shirika rasmi la habari la Saudi Arabia SPA liliripoti hivi karibuni kuwa, Riyadh itatuma ujumbe wa ngazi ya juu utakaoongozwa na Waziri wa Uchumi na Mipango wa nchi hiyo ya kifalme kwenda kushiriki mkutano huo wenye anwani bandia ya "Amani na Ufanisi" kwa Wapalestina wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Aidha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu imesema Abu Dhabi itatuma ujumbe kwenye mkutano huo wa Manama. 

Maandamano ya kupinga Muamala wa Karne

Mkutano huo ulioitishwa na Marekani umepangwa kufanyika tarehe 25 na 26 za mwezi huu ambapo katika jukwaa hilo kutatangazwa nara bandia ya 'kuvutia uwekezaji na eti kuboresha hali ya kiuchumi ya Wapalestina' katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza ambao nao uko chini ya mzingiro. 

Mpango wa Muamala wa Karne ambao unadaiwa na Wamarekani kuwa utahitimisha mzozo wa Wapalestina na Wazayuni, mbali na kufuta kabisa ndoto ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina, unawazuia pia kuunda nchi yao huru sambamba na kubariki rasmi uvamizi wa utawala wa Kizayuni na kuufanya uendelee kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.