Israel yawatia mbaroni makumi ya Wayahudi wa Kiethiopia, maandamano yashtadi
Makumi ya Wayahudi wenye asili ya Ethiopia wamekamatwa na jeshi la Polisi la utawala haramu wa Israel huku maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa polisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel yakishtadi.
Waandamanaji hao wameendelea kukabiliana na maafisa usalama wa Israel mjini Tel Aviv wakati wa maandamanao hayo ambayo hapo jana yaliingia siku yake ya tatu.
Wayahudi hao wenye asili ya Ethiopia wamesikika wakipiga nara dhidi ya Israel na kulaani ukatili wa polisi wa utawala huo. Kadhalika waandamanaji kadhaa wamejeruhiwa vibaya baada ya polisi ya Israel kutumia nguvu kupita kiasi dhidi yao.
Micky Rosenfeld, msemaji wa polisi ya utawala katili wa Israel amesema waandamanaji 130 wametiwa mbaroni kufikia sasa. Hata hivyo wanaharakati wanaoongoza maandamano hayo wamesisitiza kuwa idadi ya waandamanaji waliotiwa mbaroni ni kubwa mno kuliko iliyotajwa na polisi.
Maandamano haya yalianza Jumanne, baada ya mazishi ya kijana wa Kiyahudi mwenye asili ya Ethiopia aliyeuawa na askari polisi wa Israel hivi karibuni.
Jumapili iliyopita, polisi wa utawala wa Kizayuni walimuua kwa kumpiga risasi kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 18 kwa jina Solomon Tekah Myahudi mwenye asili ya Ethiopia katika mji wa kaskazini wa Haifa.
Wayahudi wenye asili ya Ethiopia wanaoonekana raia wa daraja la tatu wamekuwa wakiadamana mara kwa mara kupinga ukatili wa polisi ya Kizayuni dhidi yao.