Aug 09, 2019 03:01 UTC
  • BDS: Saudia inaendeleza jitihada za kuboresha uhusiano wake na Israel

Mratibu wa harakati inayopinga dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni Israel dhidi ya Wapalestina ametangaza kuwa, utawala wa Saudi Arabia unawashinikiza watu wa Palestina na kupalilia siasa za kibaguzi za Israel dhidi ya Wapalestina kwa hatua yake ya kuboresha uhusiano na utawala huo.

Mahmoud Nawajah ambaye ni mratibu wa harakati hiyo iliyopewa jina la Boycott, Divestment and Sanctions au BDS kwa kifupi, amewaambia waandishi habari kwamba, Saudia pia inafanya mikakati ya kujenga uhusiano baina ya nchi nyingine za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel na inatekeleza mpango hatari sana katika uwanja huo.

Nawajah ameashiria harakati zinazofanywa na Saudi Arabia za kujenga daraja la kurahisisha mawasiliano na ushawishi wa Israel katika eneo la magharibi mwa Asia na kusema: Riyadh pia inafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba, inasahilisha biashara baina ya utawala wa Kizayuni na nchi za kusini mwa Asia. Ameongeza kuwa, Saudia imefungua anga yake kwa shirika la ndege la Israel, EL AL ili kuzidisha ushawishi wa utawala huo katika Mashariki ya Kati.

Mratibu wa harakati ya BDS amesema kwamba, wananchi wa Saudi Arabia wanapinga suala la kuboreshwa uhusiano wa nchi yao na utawala haramu wa Israel na kusema Wapalestina wana watarajio makubwa kwa mataifa na wananchi katika nchi za Kiarabu na si watawala wao. 

Saudi Arabia inafanya jitihada za kujenga uhusiano na utawala wa Israel ambao takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwaka 1967 hadi mwaka jana wa 2018 umewaua shahidi zaidi ya Wapalestina elfu 45 na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine.      

Tags