Jeshi la Saudia lashambulia ngome ya wanamgambo wa UAE mjini Aden
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55309-jeshi_la_saudia_lashambulia_ngome_ya_wanamgambo_wa_uae_mjini_aden
Jeshi la Saudia ambalo linaongoza uvamizi dhidi ya Yemen limeshambulia ngome ya wanamgambo wanaopata himaya ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mjini Aden na kuitaja ngome hiyo kuwa 'tishio'. Hii ni katika hali ambayo UAE ni mshirika mkuu wa Saudia katika vita dhidi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 11, 2019 02:20 UTC
  • Jeshi la Saudia lashambulia ngome ya wanamgambo wa UAE mjini Aden

Jeshi la Saudia ambalo linaongoza uvamizi dhidi ya Yemen limeshambulia ngome ya wanamgambo wanaopata himaya ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mjini Aden na kuitaja ngome hiyo kuwa 'tishio'. Hii ni katika hali ambayo UAE ni mshirika mkuu wa Saudia katika vita dhidi ya Yemen.

Televisheni ya Saudia imetangaza Jumapili kuwa mashambulizi kama hayo yataendelea kutekelezwa dhidi ya ngome za wanamgambo hao wanaoungwa mkono na UAE. Taarifa ya Televiosheni hiyo imesema wanamgambo hao wa kundi la Baraza la Mpito la Kusini (STC) wanapaswa kuondoka katika eneo hilo ambalo lilikuwa linakaliwa na mrengo wa Abdu Rabbuh Mansour Hadi, rais wa Yemen aliyepinduliwa. STC ni kundi linalotaka kujitenga eneo la kusini mwa Yemen na linapata uungaji mkono wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Siku ya Jumamosi, kundi hilo lilichukua udhibiti wa 'ikulu ya rais' mjini Aden.  Mansour Hadi, anayepata himaya ya Saudia na ambaye sasa yuko uhamishoni mjini Riyadh, aliwahi kutangaza Aden kuwa makao makuu yake.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu ametaka kuanza mazungumzo kwa ajili ya kuhitimisha hali ya mvutano katika mji wa Aden na kurejesha amani kusini mwa Yemen.

Abdullah bin Zayed al Nahyan amewasilisha ombi hilo kwa Martin Griffith Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen ili atafute njia ya kusimamishwa mapigano katika mji wa Aden huko Yemen. Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati amewasilisha ombi hilo kufuatia kuongezeka hitilafu  kati ya vibaraka wanaoungwa mkono na UAE na Saudi Arabia huko Aden.