OIC: Baitul Muqaddas (Jerusalem) ni mji mkuu wa Palestina
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imesisitiza kuwa: Baitul Muqaddas utabakia daima kuwa mji mkuu wa Palestina.
OIC imetoa taarifa na kutangaza kuwa: Katika kumbukumbu ya kuchomwa moto msikiti wa Al Aqsa, uchokozi unaozidi kufanywa na Wazayuni dhidi ya mahali hapo patakatifu kwa njia ya kuwawekea vizuizi waumini wanaotaka kuingia humo kusali na uvunjiaji heshima mkubwa unaofanywa na walowezi wa Kizayuni vingali vinaendelea.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imeashiria kupanuka kwa harakati za utawala wa Kizayuni za kuchimba mashimo kandoni na chini ya msikiti wa Al Aqsa katika muendelezo wa sera za Uyahudishaji na ubadilishaji muundo wa kijiografia na wa idadi ya watu wa mji wa Baitul Muqaddas na kueleza kwamba: Hatua hiyo ni ukiukaji wa dhahiri wa sheria na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Jumuiya hiyo aidha imetilia mkazo ulazima wa kulindwa heshima ya matukufu ya Kiislamu na Kikristo katika mji huo wa Quds na uhusiano wa milele uliopo baina ya Waislamu wa kila pembe ya dunia na msikiti uliobarikiwa wa Al Aqsa.
Hujuma ya kuuchoma moto msikiti wa Al Aqsa, ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na moja ya maeneo matakatifu ya dini za mbinguni, iliyofanywa tarehe 21 Agosti 1969 ni kielelezo na ushahidi mwingine wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na doa jeusi kwa maghasibu hao wa Quds ambalo litabakia milele.
Utawala wa Kizayuni uliihusisha jinai hiyo, ambayo ilikabiliwa na hasira na ghadhabu za Waislamu duniani kote, na Dennis Michael Rohan, mtalii wa Kiyahudi mwenye misimamo ya kufurutu mpaka aliyekuwa na asili ya Australia, ambaye baada ya kumpandisha kizimbani kwenye mahakama ya kimaonyesho ulimwachilia huru kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya akili.../