Operesheni ya Uturuki imefanya watu laki 3 kuwa wakimbizi Syria
Operesheni ya kijeshi ya Uturuki huko kaskazini mwa Syria iliyopewa jina la 'Chemchemi ya Amani' imepelekea watu zaidi ya laki tatu kuyahama makazi yao na kukimbilia usalama wao.
Mkuu wa shirika linalojiita Syrian Observatory for Human Rights, Rami Abdul Rahman alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, idadi kubwa ya watu walioacha makazi yao na kukimbilia usalama wao huko kaskazini mwa Syria ni wakazi wa maeneo ya Tal Abyad, Kobane na katika mkoa wa Hasakah.
Amesema shule zaidi ya 40 zimegeuzwa kuwa vituo vya dharura vya kuwapokea wakimbizi wa ndani katika maeneo hayo.
Wakati huohuo, Jeshi la Uturuki limedai kuwa hadi sasa limeshawaangamiza magaidi 673 katika operesheni hiyo iliyoanza siku ya Jumatano ya tarehe 9 Oktoba.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter, Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imesema kwamba oparesheni hiyo itaendelea hadi pale magaidi wote watakapoangamizwa kaskazini mwa Syria.
Licha ya wasiwasi wa jamii ya kimataifa kuhusu taathira hasi za operesheni hiyo, lakini Uturuki inashikilia kuwa itaendeleza mashambulizi yake ambayo eti yanalenga tu makundi ya kigaidi ya YPG, PKK na Daesh.