Qatar yatangaza kufuta mfumo wa Kafala katika ajira
Serikali ya Qatar imeahidi kufuta mfumo wa ajira unaowabana wafanyakazi wahajiri kwa waajiri wao na kuwafanya walazimike kupata idhini ya kampuni wanazotumikia ili kuweza kuondoka nchini humo.
Waziri Mkuu wa Qatar Abdullah bin Nasir bin Khalifa Al Thani amethibitisha kwa ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ripoti kuhusu mageuzi ya sera na sheria zitakazowekwa kwa ajili ya kuboresha viwango vya huduma za kijamii kwa wafanyakazi wa vibarua na kuongeza kwamba nchi hiyo itahehshimu kikamilifu haki za msingi kuhusiana na ajira.
Chini ya mfumo wa "Kafala" wenye maana ya ufadhili, ambao umekuwa ukitumika nchini Qatar, wafanyakazi wahajiri hulazimika kupata idhini ya kutokuwa na pingamizi kutoka kwa waajiri wao (NOC) kabla ya kuhamia mahali pengine pa kazi, sheria ambayo watetezi wa haki wanasema, inawabana waajiriwa hao kwa waajiri wao na kusababisha kunyonywa na kuonewa na waajiri hao.
Qatar pamoja na sheria zake za kazi imekuwa ikifuatiliwa kimataifa tangu nchi hiyo ilipotangazwa kuwa mwenyeji wa michuano ya soka ya Kombe la Dunia ya FIFA 2022. Serikali ya Doha imeahidi kutatua mizozo inayohusu wafanyakazi wahajiri wakati inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo.
Mwezi Agosti mwaka huu kulitolewa miito mingi kuitaka Qatar "iondoe hali kutokuwepo mlingano wa mamlaka kati ya waajiriwa na waajiri wao" baada ya wafanyakazi wa vibarua wasiopungua elfu tano kuandamana nchini humo wakilalamikia ucheleweshwaji wa mishahara na mazingira yasiyoridhisha ya ufanyaji kazi.../