Oct 26, 2019 02:35 UTC
  • Watu sita watiwa mbaroni Saudia kwa kumkosoa mpambe wa Bin Salman

Wanaharakati wa haki za binaadamu nchini Saudia wameripoti habari ya kutiwa mbaroni na maafisa usalama wa nchi hiyo watu sita, kwa tuhuma ya kumkosoa mmoja wa watu wa karibu na Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na wanaharakati hao imesema kuwa watu hao waliotiwa mbaroni na maafisa usalama wa Saudia, watatu ni malenga, huku mmoja kati yao akiwa ni mwanazuoni wa kidini anayejulikana kwa jina la Sheikh Abdul Rahman Al-Mahmoud. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu hao wametiwa mbaroni baada ya kumkosoa Turki Al-Sheikh, Mkuu wa Ustawi nchini Saudia ambaye ni kati ya watu wa karibu sana na Mohammad Bin Salman, kwa kusema kuwa siasa zake zimechochea ufisadi ndani ya nchi hiyo. Wanaharakati wa haki za binaadamuu nchini Saudia wamesisitiza kwamba, kutiwa mbaroni watu hao, kumeifanya idadi ya watu waliokwishatiwa mbaroni tangu mwaka 2017 hadi sasa kwa kutoa maoni yao kufikia 110.

Sheikh Abdul Rahman Al-Mahmoud, ni mwanazuoni wa kidini kati ya watu sita waliotiwa mbaroni hivi karibuni

Mwezi Septemba 2017, miezi michache baada ya Bin Salman kuteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, makumi ya wafanyabiashara, wanazuoni wa kidini, wanawafalme, wanaharakati wa haki za binaadamu na haki za wanawake pamona na maulama wa nchi hiyo, walitiwa mbaroni na kutupwa jela. Hii ni katika hali ambayo asasi za kimataifa likiwemo Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International), Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch pamoja na Umoja wa Ulaya kwa mara kadhaa zimekuwa zikilalamikia hukumu za kifo zinazotolewa na utawala wa Aal-Saud dhidi ya raia wa nchi hiyo, hata hivyo utawala huo umeendeleza ukandamizaji wake dhidi ya wapinzani na wanaharakati wa haki za binaadamu na wa haki za wanawake nchini.

Tags