Palestina yatangaza utayarifu wa kukata kikamilifu uhusiano wake na Marekani
Rais Mahmoud Abbas wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, msimamo wa Marekani wa kuutambua ujenzi wa vitongozi vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ni halali, utapelekea kukatwa kikamilifu uhusiano wa serikali hiyo na Washington.
Abbas ameongeza kwamba tajriba ya uhusiano wa Palestina na Marekani hasa baada ya kujiri makubaliano ya Oslo, inaonyesha kwamba kamwe Washington haijawahi kuchukua hatua chanya kuhusu Palestina. Kadhalika rais huyo wa serikali ya mamkala ya ndani ya Palestina amejibu matamshi ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuhusiana na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuongeza kuwa, matamshi hayo sio jambo jipya na ni katika ukamilishaji wa hatua haribifu za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Marekani, alitangaza kwamba serikali ya Rais Donald Trump imebadili siasa zilizochukuliwa na mtangulizi wake Barack Obama wa nchi hiyo kuhusiana na suala la ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Akibainisha suala hilo Pompeo alisema kuwa, serikali ya Marekani haitambui tena shughuli za ujenzi huo haramu wa vitongoji katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ulioanza miongo kadhaa iliyopita katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na bila ya uratibu kuwa ni kinyume cha sheria. Kwa sasa utawala huo bandia unajenga vitongozi laki nne katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vitongoji laki mbili vingine katika mji wa Quds, ambapo kwa mujibu wa sheria za kimataifa ujenzi huo katika maeneo yaliyotajwa ni haramu.