Uturuki yatishia tena kufunga Kituo cha Anga cha Incirlik
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i57924-uturuki_yatishia_tena_kufunga_kituo_cha_anga_cha_incirlik
Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki kwa mara nyingine tena imetishia kwamba atafunga shughuli za majeshi ya Marekani katika Kituo cha Anga cha Incirlik nchini hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2019 23:38 UTC
  • Uturuki yatishia tena kufunga Kituo cha Anga cha Incirlik

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki kwa mara nyingine tena imetishia kwamba atafunga shughuli za majeshi ya Marekani katika Kituo cha Anga cha Incirlik nchini hiyo.

Erdogan ametoa vitisho hivyo baada ya Kongresi ya Marekani kupasisha azimio lililotambua rasmi mauaji ya kimbari ya utawala wa Otmania (Ottoman Empire) dhidi ya Waarmenia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Erdogan amesema: "Ankara yumkini ikaifungia Marekani vituo vya anga vya Incirlik na Kurecik." 

Wachambuzi wa mambo wanasema maafisa wa serikali ya Uturuki wamekuwa wakikariri vitisho vya kufunga Kituo cha Anga cha Incirlik kwa ajili ya kuwashinikiza wapinzani wake. Kabla ya hapo pia maafisa wa serikali ya Ankara walikuwa tayari wameitishia Marekani na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kwamba itawafungia kituo hicho cha anga. Kwa msingi huo inatupasa kusema kuwa, hii si mara ya kwanza kwa Ankara kutoa vitisho kama hivyo. Ankara imekuwa ikitoa vitisho kama hivyo kwa visingizio mbalimbali lakini baada ya muda suala hilo linatulia na hali inabakia kama ilivyokuwa. 

Recep Tayyep Erdogan

Kituo cha Anga cha Incirlik kilichoko katika eneo la Adana huko kusini mwa Uturuki kilianzishwa mwaka 1953 baada ya makubaliano ya Marekani na Uturuki kwa ajili ya kutumia kwa pamoja kituo hicho cha jeshi la anga. Kituo hicho ni miongoni mwa kambi muhimu za kijeshi zinazotumiwa na Marekani na nchi nyingine zenye nguvu wanachama katika Shirika na NATO dhidi ya nchi za Mashariki ya Kati.

Mwaka huu na katika kumbukumbu ya mwaka wa tatu baada ya jaribio la mapinduzi yaliyofeli nchini humo ilionekana kuwa serikali ya Uturuki imeazimia hasa kufunga kituo hicho kwa jeshi la Marekani hususan baada ya maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Adana mbele ya kituo hicho. Wakati wa maandamano hayo yaliyofanyika mwezi Julai mwaka huu, kiongozi wa Jumuiya ya Vijana ya Anatoly, Salih Turan alisema: "Kambi za majeshi ya Marekani nchini Uturuki ndizo zinazopanga na kutekeleza mapinduzi na harakati za kijeshi kama zile za mwaka 1960, 1971, 1980, 1997 na jaribio lililofeli la mapinduzi ya Julai 2016."

Abdulaziz Kranchal ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Uturuki alihutubia maandamano ya Adana na kusema: "Wahalifu wa Marekani ambao wako katika kambi 28 za NATO hususan katika kambi ya jeshi la anga ya Incirlik, wanachafua ardhi ya Uturuki ambayo ni sehemu ya ulimwengu wa Kiislamu. Askari hao wanashambulia kwa mabomu Baghdad (Iraq) na Syria kwa kutumia kambi hizo, na walishambulia Ankara nyakati za usiku katika jaribio la mapinduzi la tarehe 15 Julai."

Kambi ya jeshi la Marekani, Incirlik Uturuki

Kwa ujumla ni kwamba, licha ya tahadhari zinazotolewa na wananchi na waatalamu wa mambo wa Uturuki lakini inatupasa kusema kuwa, katika kipindi chote cha muongo mmoja uliopita Ankara imekuwa ikitumia vitisho vya kufunga shughuli za kambi ya jeshi la anga ya Incirlik kwa ajili ya kuzishinikiza nchi za Magharibi wanachama wa NATO.

Ukweli ni kwamba, tangu Recep Tayyep Erdogan aliposhika madaraka ya nchi mwaka 2002, suala la kusimamishwa Kituo cha Anga cha Incirlik limekuwa likijadiliwa mara kwa mara hususan pale serikali ya Ankara inapokabiliwa na mashinikizo ya nchi za Magharibi. Kwa msingi huo ni jambo lililo mbali kwamba maafisa wa serikali ya Uturuki watatekeleza kivitendo vitisho vya Rais Edogan vya kufunga shughuli za kituo hicho licha ya Kongresi ya Marekani kutambua rasmi mauaji ya kimbari ya Waarmenia katika Vita vya Kwanza vya Dunia.