Nchi za Kiarabu, miaka 9 baada ya kujichoma moto Bouazizi
Tarehe 17 Disemba miaka 9 iliyopita kijana muuza mboga wa Tunisia, Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto akilalamikia kitendo cha kudhalilishwa na polisi wa nchi hiyo. Tukio lilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa nchi za Magharibi.
Hivi sasa, miaka 9 baada ya Bouazizi kujichoma moto, linajitokeza swali kwamba, nchi za Kiarabu ziko katika hali gani?
Baada ya Bouazizi kujichoma moto, madikteta Zainul Abidin bin Ali wa Tunisia, Hosni Mubarak wa Misri, Muammar Gaddafi wa Libya na Abdullah Saleh wa Yemen waliondolewa madarakani. Madikteta hao wote wameaga dunia au kuuliwa isipokuwa Hosni Mubarak ndiye aliyebakia hai hadi hivi sasa. Gaddafi aliuawa mwaka 2011 katika vita vya ndani vya Libya, Abdullah Saleh aliuawa mwaka 2018 katika mlipuko wa bomu na Bin Ali ameaga dunia Septemba mwaka huu wa 2019 nchini Saudi Arabia kutokana na maradhi.
Mapinduzi ya wananchi wa Misri dhidi ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak yalizimwa au kutekwa na wanajeshi mwaka 2013 na madaraka ya nchi yanashikiliwa na kiongozi wa mapinduzi yaliyoiondoa madarakani serikali halali, Jenerali Abel Fattah al Sisi. Huko Libya pia mapinduzi ya wananchi yamepoteza mwelekeo na kuondolewa katika mkondo wake na sasa nchi hiyo imetumbukia katika vita vya ndani. Mapinduzi ya Watunisia ndiyo mfano pekee wa mapinduzi yenye mafanikio ya wananchi katika nchi za Kiarabu. Mapinduzi ya wananchi wa Yemen pia yameingia katika mkondo tofauti baada ya taifa la nchi hiyo kutwishwa vita na mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake, japokuwa mapinduzi yenyewe bado hayajapotoshwa. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, miaka 9 sasa tangu baada ya mapinduzi ya wananchi wa Yemen dhidi ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Yemen imeshuhudia mabadiliko kadhaa muhimu.
Kwanza ni kwamba, harakati ya Ansarullah na washirika wake wameunda serikali ya uokovu wa kitaifa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Sanaa na kuwa kundi la kisiasa lenye nidhamu na mpangilia madhubuti zaidi nchini Yemen. Pili ni kwamba, mashambulizi ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen yamevuruga umoja na mshikamano wa kitaifa na sasa nchi hiyo inatawaliwa na serikali kadhaa zinazodhibiti maeneo tofauti ya kijiografia.
Mbali na hayo ulimwengu wa Kiarabu hususan katika eneo la Ghuba ya Uajemi umekumbwa na mizozano, hitilafu na migawanyiko. Mhadhiri wa chuo kikuu Mahmoud Sariul Qalam anasema: "Utaifa wa Kiarabu badala ya kuwa sababu ya kuzidisha ushirikiano sasa unazidisha upinzani na uhasama baina ya nchi za Kiarabu." Mfano hai wa mizozo na uhasama huo ndani ya nchi za Kiarabu ni ule uliopo baina ya Qatar na nchi nne za Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain. Upande uliopigwa mweleka na kulazwa chali katika upinzani huu ni Saudi Arabia inayojinadi kuwa kinara wa nchi za Kiarabu. Vielelezo vya karibuni kabisa vya mivutano na mizozo hiyo ni hatua ya hivi majuzi ya Amir wa Qatar, Sheikh Tamim kususia mwaliko wa Mfalme Salman bin Abdul Azizi wa Saudi Arabia wa kushiriki mkutano wa viongozi wa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mjini Riyadh na badala yake akaamua kwenda safarini barani Afrika.
Maudhui ya tatu muhimu katika kipindi hiki cha miaka 9 baada ya kuanza mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu ni kwamba nafasi ya harakati na kambi ya mapambano na muqawama imeimarika zaidi na zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Marekani, Brian Katz anasema: "Hii leo kambi ya muqawama haiwezi tena kuitwa kambi moja bali imepanuka na kuwa umoja na mshikamano mkubwa na kuzidisha sana nguvu na uwezo wa kujilinda wa wanamuqawama."
Wakati huo huo nafasi ya Saudi Arabia kama kinara wa kundi linalopinga mapinduzi ya wananchi katika nchi za kidikteta za Kiarabu, imetetereka na kudhoofika. Hii ni kwa sababu, siasa za mabavu na vita na vilevile dharau na kiburi cha mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman kwa nchi nyingine za Kiarabu vimeaibua hali ya upinzani mkubwa katika nchi mbalimbali dhidi ya serikali ya Riyadh.
Kwa kutilia maanani haya yote tunaweza kusema kuwa, miaka 9 baada ya kuanza wimbi la mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu, Saudia inalazimika kufanya jitihada kubwa za kuboresha nafasi na sura yake ili kuzuia kushindwa na kuporomoka zaidi. Vilevile katika kipindi hiki ulimwengu wa Kiarabu umekumbwa na mizozo mingi ya kisiasa, machafuko na kudhoofika kwa misingi ya tawala katika nchi hizo.