Rais wa Iraq awasilisha barua ya kujiuzulu kwa bunge
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58131-rais_wa_iraq_awasilisha_barua_ya_kujiuzulu_kwa_bunge
Rais Barham Salih wa Iraq amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa bunge la nchi hiyo baada ya kukataa kumuidhinisha waziri mkuu mpya wa nchi hiyo kwa hoja kwamba amekataliwa na waandamanaji ambao wamekuwa wakiandamana dhidi ya serikali kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 27, 2019 03:43 UTC
  • Rais wa Iraq awasilisha barua ya kujiuzulu kwa bunge

Rais Barham Salih wa Iraq amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa bunge la nchi hiyo baada ya kukataa kumuidhinisha waziri mkuu mpya wa nchi hiyo kwa hoja kwamba amekataliwa na waandamanaji ambao wamekuwa wakiandamana dhidi ya serikali kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Barham Salih amesema kuwa anafadhilidha kujiuzulu kuliko kumteua Assad al-Eidan, aliyependekezwa na bunge la Iraq kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo kwa hoja kuwa hakubaliki na waandamanaji. Salih aliyewasilisha barua ya kujiuzulu kwa bunge la nchi hiyo hapo jana Alkhamisi amesema kuwa kutokana na kuwa katiba ya Iraq haimuruhusu kumkataa waziri mkuu aliyependekezwa na bunge, hivyo anafadhilisha kujiuzulu kuliko kumuidhinisha mtu anayepingwa na waandamanaji.

Salih amesisitiza kwamba maandamano ya wananchi yanapasa kuwafanya  wanasiasa kuzingatia maslahi ya raia kuliko maslahi yao binafsi na ya vyama wanavyoviwakilisha bungeni.

Bunge la Iraq

Wabunge sasa watakuwa na jukumu la kujadili barua hiyo ya Salih na kuipigia kura. Iwapo wataipitisha ina maana kuwa rais huyo wa Iraq atajiuzulu. Tukio hilo jipya limejiri siku moja tu baada ya bunge kumteua Assad al-Eidani mwenye umri wa miaka 59, na gavana wa zamani wa mji wa Basra na pia waziri wa zamani wa vijana na michezo, kuwa waziri mkuu mpya wa Iraq.

Wairaqi wamekuwa wakiandamana tokea terehe Mosi Oktoba wakitaka mabadiliko makubwa yafanyike serikalini kwa lengo la kuondoa ufisadi na kuboresha uchumi wa nchi hiyo. Hata hivyo maandamano hayo ambayo mwanzoni yalikuwa ya amani yamebadilika na kuwa ya ghasia na uharibifu mkubwa wa mali za umma na za watu binafsi ambapo pia mamia ya watu wamepoteza roho zao kwenye maandamano hayo.