Kushambuliwa na Marekani maeneo ya Hashdu Sha'bi nchini Iraq
Maeneo ya Hashdu Sha'bi huko al-Qaim katika mkoa wa al-Anbar yalishambuliwa na Marekani Jumapili usiku ambapo makumi ya watu waliuawa na kujeruhiwa.
Hii si mara ya kwanza kwa kambi za wapiganaji hao wa kujitolea wa Iraq kushambuliwa na Wamarekani. Kabla ya hapo, Marekani na washirika wake waliituhumu Hashdu Sha'bi kwa kupora mali, ufisadi wa kimaadili na uchochezi wa kimadhehebu, kutilia shaka mapambano yake dhidi ya magaidi wa Daesh na kuzishambulia kijeshi mara kadhaa kambi zake za kijeshi. Swali linalopaswa kuulizwa ni hili kwamba je, chanzo cha chuki hiyo yote Marekani dhidi ya Hashdu Sha'abi ni nini?
Tunaweza kusema kwamba sababu kuu ya kwanza ya uadui na chuki hiyo ni utambulisho wa Hashdu Sha'abi unaogongana moja kwa moja na wa Marekani. Jeshi la Hashdu Sha'bi ni la wapiganaji wa Kiislamu wa kujitolea nchini Iraq ambalo lina uwezo mkubwa wa kukusanya wapiganaji kwa ajili ya kufikia malengo ya mapambano ya Kiislamu katika eneo. Hii ni katika hali ambayo Marekani ni adui mkubwa wa mapambana kama hayo.
Utambulisho huo wa mapambano ya Kiislamu unaifanya Hashdu Sha'bi ipinge kila aina ya uingiliaji wa Marekani katika mambo ya ndani ya Iraq na ya eneo zima la Asia Magharibi kwa ujumla. Hashdu Sha'bi ambayo ina kambi zake za kijeshi katika eneo la al-Qaim ambalo liko karibu zaidi na kambi ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Ain al-Asad, inadhibiti na kufuatilia kwa karibu mienendo ya askari hao wa kigeni baina ya Iraq na Syria na kuwawekea vizingiti askari wa Marekani. Hashdu Sha'bi ambayo ina uhusiano mzuri na Iran ina nafasi muhimu katika matulio ya Iraq katika hali ambayo Marekani ni adui nambari moja wa Iran duniani. Baada ya kutekeleza shambulizi hilo la jana usiku dhidi ya kambi ya Hashdu Sha'abi, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza kuwa vikosi vya Hizbullah nchini Iraq vina uhusiano mkubwa na Iran.
Sababu ya pili ya uadui wa Marekani dhidi ya Hashdu Sha'bi ya Iraq ni kwa ajili ya kutetea maslahi ya utawala haramu wa Israel. Uwepo na kuimarika kwa wapiganaji hao wa kujitolea wa Kiislamu nchini Iraq kuna maana ya kuimarika ngome ya makundi ya mapambano ya Kiislamu katika eneo, jambo ambalo linagongana moja kwa moja na maslahi ya utawala ghasibu wa Israel, ambao ni mshirika muhimu zaidi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Kuhusu suala hilo. Israel Katz, Waziri wa muda wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel amekaribisha shambulizi la hivi karibuni la Marekani dhidi ya Hashdu Sha'bi na kulitaja kuwa muhimu sana.
Sababu ya tatu ya uadui wa Marekani dhidi ya Hashdu Sha'bi ni kulizuia kundi hilo la mapambano ya Kiislamu kuingizwa katika muundo mkuu wa utawala wa Iraq. Mbali na Marekani na utawala haramu wa Israel, Saudi Arabia pia ni miongoni mwa wapinzani wakuu wa kundi hilo. Hata kama Hashdu Sha'bi ni kundi la Kiarabu nchini Iraq lakini kama yalivyo makundi mengine ya Kiarabu ya Hizbullah ya Lebanon, Hamas ya Palestina na Ansarullah ya Yemen, yanatazamwa na Saudi Arabia kama makundi pinzani. Kwa msingi huo Saudia inafanya kila inaloweza kuzuia kuimarika kwa makundi kama hayo ambayo yanapingana na mitazamo na siasa zake katika eneo.
Sababu ya Nne ni kwamba Hashdu Sha'bi ina azma thabiti ya kupambana na ugaidi wa Daesh nchini Iraq katika hali ambayo Marekni si tu kwamba haina nia yoyote ya kulifuta kundi hilo la kigaidi bali inafuatilia njia za kuwaingiza tena magaidi hao nchini Iraq kutoka Syria. Kambi za Hashdu Sha'abi zilizoshambuliwa na droni za Marekani jana usiku katika eneo la al-Qaim, ni sehemu ambayo kitambo ilikuwa ikitumiwa na magaidi wa Daesh kama sehemu ya kupumzikia na kupitishia hapo mamia ya wapiganaji kutoka Syria.
Kwa ufupi hizo ndizo sababu ambazo zimeipelekea Marekani kuzishambulia kambi hizo za Hashdu Sha'abi kwa kutumia visingizio visivyo na maana.