Netanyahu anatafuta kinga ya kutopandishwa kizimbani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58268-netanyahu_anatafuta_kinga_ya_kutopandishwa_kizimbani
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa ametuma ombi kwa bunge la utawala huo, Knesset, akitaka kinga ya kutofikishwa kizimbani kuhusiana na mashtaka yanayomkabili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2020 23:20 UTC
  • Netanyahu anatafuta kinga ya kutopandishwa kizimbani

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa ametuma ombi kwa bunge la utawala huo, Knesset, akitaka kinga ya kutofikishwa kizimbani kuhusiana na mashtaka yanayomkabili.

Hivi sasa Netanyahu anakabiliwa na faili nne za ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma. Netanyahu na mke wake, Sara, wanakabiliwa na kashfa ya ufisadi inayojulikana kama '1000', ambapo wanatuhumiwa kupokea  zawadi zenye thamani kubwa zikiwemo sigara za thamani ya juu sana. Katika kashfa nyingine inyojulikana kama '2000' anatuhumiwa kufanya mazungumoa na kufukia mapatano na Arnon Mozes, mfanyabiashara na mmiliki wa gazeti la Yedioth Ahronoth ili gazeti hilo liandike habari nzuri kumhusu na mkabala wa hilo akaafiki kuliwekea vizingti gazeti la Israel Today ambalo ni mshindani mkubwa wa Yedioth Ahronoth. Netanyahu pia anakabiliwa na kashfa nyingine inayojulikana kama  '3000' inayohusu ununuzi wa nyambizi kutoka Ujerumani kwa sharti la kupokea rushwa na katika faili la nne linalojulikana kama  '4000', anakabiliwa na tuhuma za ukiukaji sheria katika  Wizara ya Mawasiliano ambapo Shirika la Mawasiliano la Bezeq lilipata faida ya dola milioni 500 kutokana na kupendelewa na serikali. Hizo ndizo kashfa za ufisadi anazokabiliwa nazo waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni.

Bunge la utawala bandia wa Israel, Knesset

Katika miaka ya hivi karibuni, mawakili wa Netanyahu na watu wenye uwezo na ushawishi mkubwa katika utawala wa Israel wamekuwa wakitumia ushawishi wao na hata vitisho ili kuhakikisha kuwa kesi hizo za ufisadi zinasitishwa au zinasimamishwa kwa muda mahakamani.

Mwanasheria mkuu wa Israel Avichai Mandelblit  alitangaza mwezi Novemba kuwa, Netanyahu amekuwa akimshinikiza sana ili asitangaze kuwa ana kesi za kujibu. Pamoja na kuwepo mashinikizo hayo, mwezi wa Novemba Mandelblit alimfungulia mashtaka Netanyahu kwa tuhuma za kupokea hongo, udanganyifu na kuvunja uaminifu. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya utawala bandia wa Israel kwa waziri mkuu aliye madakarani kufunguliwa mashtaka.

Kesi hizo za ufisadi zinazomkabili Netanyahu sasa zinatumiwa dhidi yake na vyama vya kisiasa na shakhsia mbali mbali katika utawala huo. Hivi karibuni Kanali ya 12 ya Televisheni ya Utawala wa Kizayuni ilitangaza kuwa, Rais Reuven Rivlin wa utawala wa Israel amemtaka Netanyahu ajiondoe daima katika siasa sambamba na kukiri makosa yote ambayo ameyafanya ili mkabala wa hilo asamehewe.

Bango la kumpinga Netanyahu

Pamoja na hayo, Netanyahu si tu kuwa amepinga pendekezo hilo bali amelitaka bunge limpe kinga ili mahakama zisiwe na uwezo wa kusikiliza kesi dhidi yake na hivyo aendelee kubakia madarakani.

Ombi la Netanyahu la kutaka kinga lina maana kuwa amekubali kuwa ana mashtaka ya kujibu katika kesi za ufisadi zinazomkabili. Katika upande mwingine ombi hilo lina maana kuwa Netanyahu anajaribu kukwepa kufikishwa kizimbani.

Benjamin Gantz, mwenyekiti wa chama cha  Buluu na Nyeupe katika radiamali yake kufuatia ombi la Netanyahu katika bunge la utawala huo amesema: "Kupitia ombi lake, Netanyahu ameweza kuthibitisha kuwa ana hatia na sasa anajaribu kukwepa kufikishwa kizimbani."

Nukta nyingine ni kuwa, ombi la Netanyahu la kutaka kinga ya kutoshtakiwa ni thibitisho kuwa anataka kubakia madarakani ili asijibu mashtaka ya ufisadi.

Ni wazi kuwa kutokana na kuwa Netanyahu amekuwa akishika nafasi za juu katika utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miongo kadhaa, ana ushawishi mkubwa katika muundo wa utawala huo na anajaribu kutumia ushawishi huo kuthibitisha kuwa ufisadi wa kisiasa, kiidara na kiuchumi umekita mizizi katika utawala huo bandia wa Israel.

Hivi sasa Netanyahu anafuatilia maslahi yake binafsi na hii ni nukta ambayo huko nyuma iliwahi kuashiriwa na Avigdor Lieberman, kinara wa chama cha Yisrael Beitenu.