Hizbullah: Luteni Jenerali Qassim Soleimani alikuwa kamanda wa ulimwengu wa Kiislamu
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani hakuwa kamanda wa Iran tu bali alikuwa kamanda wa ulimwengu wa Kiislamu na kambi ya muqawama dhidi ya wavamizi na mabeberu wa dunia.
Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Manar muda mfupi baada ya kuhani nyumbani kwa shahidi Haj Qassim Soleimani na kueleza kwamba, maadui wanajidanganya kwa kudhani kwamba, kwa kumuua jenerali huyo wameondoa kizingiti kikubwa, lakini muda si mrefu watafahamu kwamba, hilo litapelekea kudhihiri vikosi vyenye nguvu ambavyo vitaendeleza njia ya shahidi huyu.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameeleza kwamba, Marekani inafanya kosa kubwa kwa kudhani kwamba, kwa kumuua Luteni Jenerali Qassim Soleimani itaweza kuvuruga mahesabu na kuyafanya yawe kwa maslahi yake.
Aidha kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati yao sasa inahisi kuwa na majukumu mazito na makubwa zaidi baada ya kuuawa Luteni Jenerali Qassim Soleimani.
Wakati huo huo, shakhsia, wasomi, maulamaa, wanaharakati na viongozii wa nchi mbalimbali wameendelea kulaani mauaji yaliyofanywa na Marekani siku ya Ijumaa dhidi ya Luteni Jenerali Qassemi Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Mohandes, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Al Hashd al Shaabi).