HAMAS: Utawala wa Kizayuni unataka kuangamiza kizazi kizima cha Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58439-hamas_utawala_wa_kizayuni_unataka_kuangamiza_kizazi_kizima_cha_wapalestina
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Wazayuni wanaendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan lengo likiwa ni kuangamiza kabisa kizazi cha Wapalestina kwenye eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2020 04:34 UTC
  • HAMAS: Utawala wa Kizayuni unataka kuangamiza kizazi kizima cha Wapalestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Wazayuni wanaendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan lengo likiwa ni kuangamiza kabisa kizazi cha Wapalestina kwenye eneo hilo.

Hazem Qassem amesema hayo na kuongeza kuwa, matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni, Naftali Bennet, ya kutaka kuharakishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni sehemu ya njama mpya za Israel za kumaliza kizazi cha Wapalestina kwa msaada wa Marekani.

Ameongeza kuwa, kuendelea jinai za Israel za kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kunalifanya suala la kuchukuliwa maamuzi ya pamoja ya Wapalestina kuwa jambo la dharura zaidi.

Msemaji huyo wa HAMAS vile vile ameitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuacha kushirikiana kiusalama na jeshi la Israel na isizuie harakati za makundi ya muqawama wa Palestina.

Moja ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

 

Amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina wataendelea na mapambano yao hadi watakapowafurusha Wazayuni wote katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu na kuunda nchi ya Palestina ambayo mji mkuu wake utakuwa na Bayatul Muqaddas.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 23 Disemba 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 la kuutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uache mara moja kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina.

Hata hivyo utawala huo pandikizi kwa uungaji mkono wa baadhi ya madola ya kibeberu hasa Marekani, umedharau kabisa azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.