Harakati ya Ansarullah ya Yemen: Mchango mzuri wa Sultan Qaboos hautasahaulika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58456-harakati_ya_ansarullah_ya_yemen_mchango_mzuri_wa_sultan_qaboos_hautasahaulika
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema katika salamu za rambirambi alizotoa kufuatia kifo cha mfalme wa Oman Sultan Qaboos bin Said Al Said, kwamba kiongozi huyo alitoa mchango mzuri na chanya katika matukio ya eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 12, 2020 03:37 UTC
  • Harakati ya Ansarullah ya Yemen: Mchango mzuri wa Sultan Qaboos hautasahaulika

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema katika salamu za rambirambi alizotoa kufuatia kifo cha mfalme wa Oman Sultan Qaboos bin Said Al Said, kwamba kiongozi huyo alitoa mchango mzuri na chanya katika matukio ya eneo la Asia Magharibi.

Katika ujumbe huo wa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Oman, Muhammad Abdussalam amesema: "Wayemen hawatasahau katu mchango chanya wa aliyekuwa mfalme wa Oman Sultan Qaboos, kwa msimamo wake wa kupinga uvamizi dhidi ya Yemen na kuwaunga mkono wananchi wa Yemen."

Aidha Abdussalam amesisitiza kuwa, Wayemen wana uhakika Sultan Haitham ataendeleza njia ya Sultan Qaboos kwa hekima na uwezo kamili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif, naye pia ametuma ujumbe wa mkono wa pole wa lugha ya Kiarabu kufuatia kuaga dunia mfalme wa Oman Sultan Qaboos bin Said Al Said akikielezea kifo chake kuwa ni hasara kubwa kwa eneo.

Katika ujumbe wake huo, Zarif ametuma salamu za pongezi pia kwa Haitham bin Tariq kwa kuchaguliwa kuwa mfalme mpya wa Oman.

Ofisi ya Ufalme wa Oman usiku wa kuamkia jana ilitangaza kuwa mfalme wa nchi hiyo Sultan Qaboos bin Said ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 79.

Sultan Qaboos ameiongoza Oman kwa muda wa karibu miaka 50.

Al Marhum Sultan Qaboos bin Said Al Said 

Katika siasa na sera za nje za Oman, Sultan Qaboos alitoa kipaumbele cha kwanza kwa masuala ya amani na uthabiti, hususan wa eneo la Asia Magharibi.

Sultan Qaboos anatajwa kama "mtawala wa misimamo ya kadiri na wastani" ambaye alikuwa na nafasi muhimu katika usuluhishi na upatanishi ndani ya eneo na baina ya nchi za eneo na madola makubwa ajinabi ya nje ya eneo hili.../