Hizbullah Iraq: Muqawama unajiandaa kutoa jibu kali kwa jinai za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58502-hizbullah_iraq_muqawama_unajiandaa_kutoa_jibu_kali_kwa_jinai_za_marekani
Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Iraq amesema kuwa, kambi ya muqawama kwa makundi yake yote inajiandaa kutoa jibu kali kwa jinai za Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2020 01:19 UTC
  • Hizbullah Iraq: Muqawama unajiandaa kutoa jibu kali kwa jinai za Marekani

Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Iraq amesema kuwa, kambi ya muqawama kwa makundi yake yote inajiandaa kutoa jibu kali kwa jinai za Marekani.

Muhammad Muhyi, ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al Mayadeen ya Lebanon na kuongeza kwamba hakuna njia nyingine ghairi ya kukabiliana ana kwa ana na askari vamizi wa Marekani walioko Iraq na kwamba kambi ya muqawama imejiweka tayari kikamilifu katika maeneo mengi ya Iraq kwa ajili ya kukabiliana na askari hao wa Marekani. Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Iraq amesisitiza kwamba serikali ya Baghdad ni lazima itumie nyenzo zake zote ili iwatimue haraka askari hao vamizi wa Marekani kutoka Iraq. Sambamba na kubainisha kwamba makundi yote ya Iraq yanakiri juu ya nafasi chanya ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC katika kuihami nchi hiyo ya Kiarabu na kuwashinda magaidi wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS), Muhammad Muhyi amefafanua kwamba hakuna Muiraki yeyote anayeweza kusahau nafasi ya shakhsia huyo mwanamapambano na kushiriki kwake katika safu ya mbele katika vita vya kuwaangamiza magaidi.

Muhammad Muhyi, Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Iraq 

Usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 mwezi huu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye alikuwa ameelekea nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, akiwa pamoja na Naibu Mkuu wa harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi Abu Mahdi Al-Muhandis na wanamuqawama wengine wanane waliuliwa shahidi baada ya msafara wa magari yaliyowabeba kulengwa na makombora ya majeshi ya kigaidi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Katika kujibu jinai hiyo ya kigaidi ya Marekani, siku ya Jumatano iliyofuatia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilishambulia kwa makumi ya makombora kambi za jeshi la Marekani katika mkoa wa Al-Anbar na Erbil nchini Iraq.