Jan 20, 2020 13:14 UTC
  • Jasusi mmoja wa Marekani atiwa mbaroni mjini Beirut, Lebanon

Maafisa usalama wa Lebanon wamemtia mbaroni mwandishi mmoja wa habari wa Kimarekani katika maandamano ya wananchi mjini Beirut kwa tuhuma za kuufanyia ujasusi utawala haramu wa Kizayuni.

Mwandishi huyo wa habari ambaye hadi sasa bado hajatajwa jina, alitiwa nguvuni na maafisa usalama Jumapili ya jana wakati akichukua video za mapigano karibu na bunge la Lebanon katikati mwa mji wa Beirut. Kwa mujibu wa habari hiyo, mwandishi huyo wa Kimarekani alikuwa akichukua video na kuzituma moja kwa moja kwa gazeti la Haaretz la Kizayuni. Duru mpya ya maandamano nchini Lebanon ilianza tarehe 13 Januari mwaka huu, ambapo waandamanaji wameitisha maandamano zaidi dhidi ya serikali na kuyataja kuwa 'Wiki ya Hasira.'

Ghasia za maandamano mjini Beirut, Lebanon

Maandamano ya hivi karibuni nchini Lebanon yameandamana na ghasia kati ya polisi na waandamanaji, kiasi kwamba makumi ya watu wamejeruhiwa na wengine kutiwa mbaroni. Kufuatia ghasia hizo maafisa usalama wamewataka waandamanaji kutoyabadilisha maandamano na mikusanyiko yao kuwa ya utumiaji mbavu ukiwemo urushaji mawe, kufunga barabara na kuchoma moto matairi ya magari na vyombo vya kuhifadhia taka, la sivyo, watalazimika kutumia sheria dhidi yao.

Tags