Muamala wa Karne wa Donald Trump na matokeo yake
Rais wa Marekani amesema kuwa, siku chache zijazo atauzindua rasmi mpango wa "Muamala wa Karne."
Muamala wa Karne ni mpango wa Marekani wa eti kutatua mivutano baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel. Huko nyuma pia serikali ya Marekani imejaribu mara kadhaa kutangaza mpango huo lakini mara zote imekuwa ikifeli kutokana na sababu mbalimbali ukiwemo mgogoro mkubwa wa kisiasa ulioukumba utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa.
Muamala wa Karne ni mapango wa kidhalimu na kibaguzi kikamilifu ambao haukuangalia kitu kingine isipokuwa tu kulinda manufaa ya utawala wa Kizayuni. Kufikia hapa tulipo leo hii, tayari muamala huo umeshapelekea kutangazwa mji mtakatifu wa Quds kuwa eti mji mkuu wa Israel. Hata Marekani imehamishia mjini humo ubalozi wake uliokuweko Tel Aviv. Dhulma nyingine ya muamala huo wa kishetani ni kuwapiga marufuku wakimbizi wa Palestina wasirejee kabisa katika ardhi zao pamoja na kulipokonya silaha kikamilifu taifa hilo linalodhulumiwa kila upande.
Inavyoonekana ni kwamba, nia ya Trump ya kuuzindua Muamala wa Karne ni kuweka hadharani sura nyingine ya kibaguzi na kidhulma ya mpango huo. Lengo la hatua hiyo ya Trump ni kutaka kuukabidhi kikamilifu utawala wa Kizayuni, vitongoji vinavyozozaniwa baina ya Wapalestina na Israel. Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu na Benny Gantz, Mkuu wa Muungano wa Buluu na Nyeupe siku chache zilizopita walidai kuwa watachukua hatua maalumu za kuviunganisha vitongoji vya Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kama njia ya kuitia nguvu Israel.
Amma suala muhimu hapa ni wakati huu uliochaguliwa na Donald Trump kutangaza mpango wake wa kidhulma wa Muamala wa Karne. Mpango huo utatangazwa wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel umekwama kwenye kinamasi cha mgogoro mkubwa mno wa kisiasa.
Mpango huo umepangwa kuzinduliwa wakati huu ambapo katika upande mmoja mchakato wa kusailiwa na ikiwezekana kuuzuliwa urais Donald Trump ukiwa unaendelea katika Baraza la Sanate la Marekani na katika upande wa pili mwaka huu wa 2020 Trump ana kibarua kigumu cha kukabiliana na chama cha Democrats katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani. Trump anaona kuwa kitu pekee kinachoweza kumuokoa ni uungaji mkono wa lobi za Mayahudi nchini Marekani. Hivyo ameamua kutumia wakati huu kutangaza mpango wa kidhalimu na kibaguzi wa Muamala wa Karne ili kuvutia uungaji mkono wa Wazayuni na kupunguza mashinikizo ya ndani ya Marekani.
Suala jingine ni kwamba kuzinduliwa mpango huo kutakuwa na matokeo mengine mengi. Rais wa Marekani anadai kuwa, awali Wapalestina wataukataa mpango huo, lakini mwisho wataukubali tu. Hata hivyo tofauti kabisa na madai hayo ya Trump, njama za kutangaza mpango huo mpya zimezidisha mapigano na mivutano baina ya Wapalestina na Israel na hali imezidi kuwa mbaya.
Madhara mengine ya mpango huo ni kwamba muundo wa kijiografia wa Asia Magharibi nao utabadilika. Sababu yake ni kwamba kwa mujibu wa mpango huo, ardhi zote zinazozozaniwa baina ya Palestina na Israel na baina ya Syria na utawala wa Kizayuni, zitakabidhiwa kwa Israel. Hivyo eneo la kijiografia la Palestina na Syria litakuwa dogo huku ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel zikiwa pana zaidi. Bila ya shaka hiyo ni sababu nyingine ya kushadidi mapigano katika eneo la magharibi mwa Asia kutokana na chokochoko hizo za Kizayuni.
Nukta ya mwisho kwa leo ni kwamba nia ya Donald Trump ya kuuzindua Muamala wa Karne kwa mara nyingine inathibitisha kuwa hajali maamuzi ya jamii ya kimataifa wala maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro uliopo baina ya Palestina na Israel.