Tisho la Erdoğan kuishambulia kijeshi Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58904-tisho_la_erdoğan_kuishambulia_kijeshi_syria
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametishia kuishambulia kijeshi Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2020 22:59 UTC
  • Tisho la Erdoğan kuishambulia kijeshi Syria

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametishia kuishambulia kijeshi Syria.

Erdoğan alisema Ijumaa kuwa, Uturuki inataka kuimarisha usalama na uthabiti wa Syria na kwamba haitasita kutumia kila njia hata ikiwa ni nguvu za kijeshi katika kufikia lengo hilo. Akiashiria kwamba serikali ya Ankara haiwezi kutofautisha hali ya mambo ya mkoa wa Idlib na maeneo mengine ya Syria, amedai kuwa Uturuki ilitiliana saini na Russia makubaliano ya kuzuia mashambulizi katika mkoa huo sambamba na kuunga mkono uthabiti na juhudi za kisiasa, lakini eti serikali ya Damascus imekuwa ikikiuka mapatano hayo. Matamshi hayo ya Rais Recep Tayyip Erdoğan yametolewa katika hali ambayo siku chache zilizopita jeshi la Syria katika radiamali yake kwa hatua za makundi ya kigaidi za kukiuka mara kwa mara usitishaji vita katika mkoa wa Idlib, lilianzisha operesheni katika eneo hilo na hadi sasa limeweza kukomboa baadhi ya maeneo ya mkoa huo kutoka mikononi mwa magenge hayo ya kigaidi. Idlib ni ngome ya mwisho ya makundi ya kigaidi ya Syria ambapo kukombolewa kwake na baadhi ya maeneo ya magharibi ya mkoa wa Aleppo na mashariki mwa Latakia, kutawaweka pagumu magaidi nchini humo.

Licha ya njama za maadui wa Syria, lakini nchi hiyo inaendelea kupata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya magaidi

Badala ya matamshi ya rais wa Uturuki kuwa moja ya njia za utatuzi wa mgogoro wa Syria, yamekuwa ni aina fulani ya ukwamishaji mambo katika mgogoro huo. Hii ni kusema kuwa Uturuki tangu ulipoanza mgogoro wa ndani ya Syria, imekuwa moja ya nchi zinazounga mkono na kutoa mafunzo kwa makundi ya kigaidi, kwa madhumuni ya kuifanya nchi hiyo ya Kiarabu kutokuwa na amani. Makundi hayo ambayo yameweka wazi mahusiano yao na kundi la kigaidi la Al-Qaidah, pia hayajawahi kuficha mahusiano yao na makundi mengine ya kigaidi yanayotenda jinai. Pamoja na hayo hatua hiyo ya Uturuki imeiingiza Ankara katika mzozo wa muda mrefu nchini Syria ambapo katika kuendelea kuchochea mzozo huo, Ankara kupitia uungaji mkono wake wa kifedha na silaha kwa makundi ya kigaidi, imekuwa ikikiuka wazi sheria na mikataba ya kimataifa na haki ya kujitawala taifa hilo la Kiarabu. Uturuki inadai kuwa na wasi wasi juu ya uthabiti wa kaskazini mwa Uturuki, katika hali ambayo yenyewe imekuwa ikiwaunga mkono magaidi na hata kuchukua hatua ya kuyavamia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Rais Bashar al Assad wa Syria akifuatilia maendeleo ya vita dhidi ya magaidi

Hii ni kusema kuwa kukubaliwa kuwepo makundi ya kigaidi na askari wa kigeni katika ardhi ya Syria na kitendo cha kuigawa nchi hiyo kinyume cha sheria, ni jambo linalokwenda kinyume kabisa na misingi ya kujitawala nchi hiyo. Kwa kutilia maanani mgogoro wa sasa katika eneo, ni muhimu kwa serikali ya Uturuki kujikita zaidi katika kuimarisha mshikamano wa eneo kupitia kupambana na ugaidi, kupunguza mizozo kati ya nchi jirani na kufanya juhudi kwa ajili ya kurejesha usalama na amani ndani ya nchi hiyo kupitia ushirikiano na serikali ya Damascus. Hii ni kwa kuwa tajriba ya eneo hili imethibitisha kwamba mizozo kati ya nchi za eneo, haijawahi kusaidia utatuzi wa migogoro iliyopo katika eneo.