Wakati serikali iliyojiuzulu ya Yemen inapolazimika kukiri kufeli makubaliano ya Riyadh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59082-wakati_serikali_iliyojiuzulu_ya_yemen_inapolazimika_kukiri_kufeli_makubaliano_ya_riyadh
Rajih Badi, msemaji wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen amekiri kwamba makubaliano ya Riyadh ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo yamefeli na yamevunjika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2020 04:10 UTC
  • Wakati serikali iliyojiuzulu ya Yemen inapolazimika kukiri kufeli makubaliano ya Riyadh

Rajih Badi, msemaji wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen amekiri kwamba makubaliano ya Riyadh ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo yamefeli na yamevunjika.

Makubalino hayo ya Riyadh yaliyosimamiwa na Saudi Arabia yalifikiwa mwezi Novemba 2019 baina ya Baraza la Mapito la Kusini (STC) na serikali ya zamani ya Yemen iliyojiuzulu.

Makubaliano hayo yalitiwa saini katika mazingira ambayo mosi mapigano yalikuwa yanaendelea baina ya Baraza la Mpito la Kusini na wapiganaji wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen na pili mzozo baina ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ulikuwa umepamba moto huko kusini mwa Yemen. Hivyo lengo la makubaliano hayo lilikuwa ni kukomesha mapigano na mizozo hiyo na kuunda serikali mpya kusini mwa Yemen kwa kushirikishwa Baraza la Mpito la Kusini (STC).

Wanajeshi vamizi wa Imarati nchini Yemen

 

Ijapokuwa tangu mwanzo ilionekana wazi kwamba utekelezaji wa vipengee vya makubaliano hayo litakuwa jambo zito, lakini Wasaudia waling'ang'ania kufikiwa mapatano hayo. Hivi sasa baada ya kupita takriban miezi mitatu tangu kufikiwa makubaliano hayo, msemaji wa serikali iliyojiuzulu, Rajih Badi amejitokeza hadharani na kutangaza rasmi kufeli mapatano hayo. Ijapokuwa Badi amezilaumu Imarati na Baraza la Mpito la Kusini kutokana na kufeli makubaliano hayo, lakini kuna uwezekano wa kuweko sababu nyingine zilizopelekea kuvunjika maafikiano hayo.

Sababu ya kwanza inahusiana na vipengee vyenyewe vya mapatano hayo. Katika makubaliano hayo imeafikiwa kwamba kuundwe serikali mpya yenye mawaziri 24 na kushirikishwa Baraza la Mpito la Kusini kwenye serikali hiyo. Hayo yaliafikiwa bila ya kuzingatia kuwa, chama cha al Islah chenye misimamo ya Ikhwanul Muslimin hakikupewa nafasi maalumu kwenye serikali hiyo kama ambavyo pia hakukutolewa ufafanuzi wowote kuhusu namna wizara za serikali hiyo mpya zitakavyogawanywa. Jambo hilo lenyewe lilikuwa sababu ya kuzuka malalamiko na shutuma nyingi kutoka kwa wajumbe wa serikali iliyojiuzulu ya Abdu Rabbuh Mansour Hadi.

Sababu ya pili inahusiana na kuingizwa wanajeshi wa Baraza la Mpito la Kusini (STC) katika vikosi vya Wizara ya Ulinzi ya serikali iliyojizulu. Kifungu hicho kilikuwa na maana ya kupokonywa silaha zote Baraza la Mpito la Kusini  ili lisiwe na uwezo wowote wa kujihami. Ijapokuwa kidhahiri baraza hilo lilikubaliana na suala hilo, lakini kila kitu kilikuwa wazi tangu zamani kwamba kipengee hicho kisingeliweza kutekelezwa, na kamwe baraza hilo lisingelikubali kupokonywa silaha. Inaonekana ni kwa sababu hiyo ndio maana msemaji wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen, Rajih Badi, akasema kuwa, Baraza la Mpito la Kusini limehusika katika kuvunjika makubaliano ya Riyadh.

Mansour Hadi na wavamizi wa Yemen

Baraza hilo la STC lililizuia jeshi la Mansour Hadi kuvuuka eneo linalodhibitiwa na baraza hilo kinyume na vipengee vya mapatano ya Riyadh. Hatua hiyo ya Baraza la Mpito la Kusini lilizusha wimbi jipya la machafuko na ugomvi baina yake na serikali ya Mansour Hadi. Hata Saleh al Jubwani, waziri wa uchukuzi wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen alionesha kukasirishwa sana na jambo hilo na kufikia hadi ya kusema kwamba, watawasambaratisha waasi wa kundi la Imarati huko Aden. 

Sababu ya tatu iliyopelekea kuvunjika makubaliano ya Riyadh ni uingiliaji wa Saudi Arabia na Imarati katika masuala ya ndani ya Yemen. Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa upatanishi wa Saudia na kwa ridhaa ya Imarati. Kusema kweli mapatano hayo ya Riyadh ni sehemu ya mpango wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu wa kuigawa vipande vipande Yemen ili waidhibiti wanavyotaka. Lakini Wayemen wengi wameyapinga makubaliano hayo wakisisitiza kuwa yanavunja haki yao kuu ya kujiamulia wenyewe mambo yao.

Nukta ya mwisho tunayopenda kuigusia hapa ni kwamba, kuvunjika makubaliano ya Riyadh kuna maana ya kufeli Saudi Arabia na uwezekano wa kupamba moto upya mapigano na mizozo huko kusini mwa Yemen.