Serikali ya Misri: Watakaopinga mpango wa Muamala wa Karne watakiona
Serikali ya Misri imetoa onyo kali kwa shakhsia na wanadiplomasia wa nchi hiyo wanaoukosoa mpango wa Muamala wa Karne na kueleza kwamba, watakaoupinga mpango huo watakaiona.
Tayari serikali ya Misri imechukua hatua ya awali ambapo imewaita na kuwaonya wanasiasa, wanadiplomasia na shakhsia wa nchi hiyo wanaoukosoa mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne na kuwaonya kuhusiana na matokeo mabaya ya kuupinga mpango huo.
Taarifa kutoka Misri zinasema kuwa, vyombo vya kijasusi vya nchi hiyo vinafuatilia kwa karibu mijadala na makala mbalimbali katika mitandao ya kijamii na kuorodhesha majina ya wanadiplomasia na shakhsia wa nchi hiyo wanaoukosoa mpango huo, hususan wanaokosoa msimamo wa serikali ya Rais Abdul-Fattah al-Sisi kuhusiana na mpango wa Muamala wa Karne.
Ikumbukwe kuwa, Jumanne ya tarehe 28 Januari, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.
Wakati serikali ya Misri ikitoa onyo hilo, maeneo mbalimbali ulimwenguni yameendelea kushuhudia maandamano ya kulaani na kupinga mpango huo wa Muuamala wa Karne unaokanyaga wazi haki za Wapalestina.