Kamatakamata ya wanawafalme Saudia imetokana na kudhoofika hali Mfalme Salman
Chanzo cha habari cha kuaminika kimearifu kuwa, wimbi jipya la kamatakamata linalofanywa na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman limesababishwa na kuzidi kuwa mbaya hali ya kiafya ya Mfalme Salman bin Abdulaziz wa nchi hiyo ambaye anaugua ugonjwa wa kusahau na kupoteza kumbukumbu (Alzheimer's disease).
Duru hizo za habari zimeliambia gazeti la Quds Al-Arabi Jumamosi kuwa, Bin Salman amevuka mistari yote miekundu ya Ukoo wa Kifalme wa Saudia kutokana na kudhoofika kwa hali ya Mfalme Salman mwenye umri wa miaka 84.
Utawala wa Aal-Saud umemtia nguvuni Mwanamfalme Ahmed bin Abdulaziz Aal-Saud, ndugu wa Mfalme Salman pamoja na mpwa wa mfalme huyo Muhammad bin Nayef katika muendelezo wa kampeni inayoendeshwa na Bin Salman ya kuwakandamiza jamaa wa aila hiyo ya kifalme ili kujisafishia njia ya kushika hatamu za ufalme wa nchi hiyo baada ya baba yake.
Chanzo hicho cha habari kimeliambia gazeti la Quds Al-Arabi kuwa, simu za wanawafalme hao zimezimwa huku mawasiliano yao ya nje ya nchi yakikatwa pia katika kipindi cha siku mbili zilizopita.
Inaarifiwa kuwa, kutokana na ukongwe na uzee unaomuandama Mfalme Salman, mwanawe Bin Salman ameelemewa na majukumu na kushindwa kudhibiti hali ya kisiasa na kiusalama ndani ya utawala huo, na yeyote anayefuatilia au kukosoa udhaifu huo anaswekwa ndani.
Muhammad bin Nayef ambaye alikuwa na nafasi ya mbele ya kurithi kiti cha ufalme, alikuwa pia waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo kabla ya kuvuliwa wadhifa huo mwaka 2017. Baadaye mwaka huo, wanawafalme na wanasiasa mashuhuri zaidi ya 200 wa Saudia walitiwa nguvuni na kuwekwa kizuizini kwa amri ya Muhammad bin Salman, miongoni mwao akiwemo bilionea mwanamfalme Alwaleed bin Talal, ambaye alishikiliwa kwenye hoteli ya Ritz Carlton.