Uturuki yakiri kuongezeka hasara za kijeshi nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59627-uturuki_yakiri_kuongezeka_hasara_za_kijeshi_nchini_syria
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amekiri juu ya hasara za kiroho na mali za jeshi la nchi yake huko katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria kufuatia mapigano makali kati ya askari wa nchi mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 08, 2020 23:29 UTC
  • Uturuki yakiri kuongezeka hasara za kijeshi nchini Syria

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amekiri juu ya hasara za kiroho na mali za jeshi la nchi yake huko katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria kufuatia mapigano makali kati ya askari wa nchi mbili.

Rais Erdoğan aliyasema hayo akiwa njiani kutoka Moscow, Russia ambapo amekiri kwamba katika mapigano ya askari wa Uturuki na Syria katika mkoa wa Idlib, serikali Ankara imepata hasara kubwa ambayo inafikia mamia ya askari. Aidha amekiri kwamba lengo pekee la nchi yake katika kuongeza harakati za kijeshi nchini Syria, ni kupinga serikali inayotawala Damascus. Matamshi hayo ya rais wa Uturuki yametolewa katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni viongozi wa serikali ya Ankara walitoa idadi isiyo sahihi kuhusu hasara waliyoipata Syria kwa lengo la kupotosha fikra za walio wengi nchini Uturuki. Tangu miezi miwili iliyopita jeshi la Syria lilianzisha operesheni za kuusafisha mkoa wa Idlib kutokana na magenge ya magaidi. Licha ya kwamba operesheni hizo za jeshi la Syria zililenga mabaki ya magaidi katika mkoa wa Idlib, lakini idadi kubwa ya askari wa jeshi la Uturuki nao walikuwa miongoni mwa magaidi hao na hivyo kuathirika kutokana na operesheni hizo. Ukweli ni kwamba, imebainika kuwa askari wa Uturuki wako Syria kwa lengo la kutoa msaada wa kijeshi, kifedha na hata mafunzo ya kijeshi kwa magaidi. Inaonekana kwamba wasi wasi wa viongozi wa Uturuki kuhusiana na operesheni za jeshi la Syria dhidi ya magaidi wa mkoa wa Idlib, zinahusiana na suala hilo.

Uvamizi wa Uturuki nchini Syria imekuwa na matokeo kinyume

Ukweli ni kwamba viongozi wa serikali ya Erdogan wanajitahidi kuzuia operesheni za jeshi la Syria dhidi ya Magaidi, hata hivyo mikataba ya kimataifa na hata wale walio na maslahi huko Syria, wanatambua vyema kuwa kutekelezwa operesheni dhidi ya makundi ya kigaidi, ni haki ya serikali halali ya Damascus. Kwa mfano, baada ya kikao cha viongozi wa Russia na Uturuki mjini Moscow, Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia kupitia kikao na waandishi wa habari alisema: "Syria inayo haki ya kuyasambaratisha kikamilifu magaidi ndani ya ardhi yake." Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia alisisitiza kwamba: "Kusambaratishwa makundi ya kigaidi nchini Syria ni suala la dharura na msimamo wa serikali ya Moscow kuhusiana na suala hilo upo imara na wala haujabadilika. Aliongeza kwamba kwa mara nyingine katika makubaliano ya hivi karibuni ya usitishaji vita mkoani Idlib kati ya viongozi wa Ankara na Moscow, kulisisitizwa kuendelezwa mapambano dhidi ya ugaidi kwa namna yoyote ile." Alkhamisi iliyopita viongozi wa Russia na Uturuki walikutana mjini Moscow ambapo baada ya masaa kadhaa ya mazungumzo, walifikia makubaliano kuhusu usitishaji vita mkoni Idlib. Miaka kadhaa iliyopita wanasiasa waungaji mkono na wapinzani wa serikali ya Ankara na walisisitizia umuhimu wa kuondoka askari wa Uturuki kutoka Syria sambamba na kurejeshwa uhusiano mwema kati ya Ankara na serikali halali ya Rais Bashar al-Assad. Katika uwanja huo weledi wa masuala ya kisiasa nchini Uturuki pia sambamba na kuzitaja kuwa zisizo sahihi siasa za serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar, wametaka kubadilishwa siasa hizo mara moja. Katika uwanja huo Siddiki Zabalan, wakili na mtaalamu mashuhuri wa Uturuki katika masuala ya kisiasa amezungumzia uvamizi wa kijeshi wa Uturuki ndani ya ardhi ya Syria kwa kusema: "Serikali ya Uturuki ni lazima iangalie upya siasa zake na ihitimishe uvamizi wake huo."

Malengo ya Uturuki ndani ya Syria yamegonga mwamba

Mtaalamu huyo wa Uturuki pia ameashiria makosa ya mara kwa ya chama tawala nchini Uturuki kuhusiana na Syria na kuongeza kwamba: "Makundi ya wabeba silaha yanayoungwa mkono na Uturuki nchini Syria, ni magaidi halisi wanaotumia jina la Uislamu kutenda jinai zisizohesabika." Kiujumla ni kwamba kwa kuzingatia ukosoaji wa mara kwa mara wa wanasiasa na wataalamu wa Uturuki kuhusu siasa mbovu za serikali ya Rais Tayyip Erdoğan ni lazima tuseme kwamba, maslahi ya kitaifa ya Uturuki yatakuwa chanya wakati ambao nchi hiyo itafanya haraka kuhitimisha uvamizi wake nchini Syria na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Damascus. Ni suala lililo wazi kwamba kinyume na hali hiyo, serikali ya Erdoğan itaendelea kuwa wenzo wa kutekeleza malengo ya Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel nchini Syria.