Saudia yazuilia maiti 90 za wanaharakati na wakosoaji wake
Utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia unazuilia zaidi ya maiti 90 za wanaharakati waliouawa katika mazingira ya kutatanisha, wakiwemo wakosoaji wa mradi tata wa mabiioni ya dola katika pwani ya Bahari Nyekundu.
Mtandao wa habari wa Mirat al-Jazeera umeripoti kuwa, utawala wa Riyadh umekataa kata kata kukabidhi miili hiyo ya wanaharakati na wakosoaji waliouawa katika mazingira ya kutatanisha kwa familia zao.
Miongoni mwa maiti hizo ni ya mwanaharakati mashuhuri, Abdul-Rahim al-Howeiti, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na maafisa usalama wa Aal-Saud katika mji wa al-Khuraybah, kaskazini magharibi mwa eneo la Tabuk mapema mwezi huu.
Mwanaharakati huyo amekuwa akituma mitandaoni jumbe za video za kupinga mradi wa dola bilioni 500 wa Neom katika pwani ya Bahari Nyekundu, uliosababisha wakazi wa eneo hilo kufurushwa na vyombo vya dola ili kupisha ujenzi huo tata.
Ripoti ya mtandao wa habari wa Mirat al-Jazeera haijabainisha iwapo wanaharakati hao 90 waliuawa na maafisa usalama katika maandamano ya kupinga mradio huo au la.
Haya yanajiri siku chache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International kusema kuwa, utawala wa Aal-Saud mwaka jana ulivunja rekodi ya kutekeleza hukumu ya kuwanyonga watu ndani ya mwaka mmoja nchini Saudi Arabia.
Katika ripoti yake mpya, Amnesty imesema mwaka jana 2019 utawala wa Riyadh uliwanyonga watu 184 wakiwemo wanawake sita, ambapo karibu nusu yao ni raia wa kigeni.