Saudia yatupilia mbali maombi yanayoitaka kuwaachia huru wafungwa wa Kipalestina
Watawala wa Saudi Arabia na licha ya matakwa ya kila mara ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), asasi za haki za binaadamu na familia za watu wanaoshikiliwa huko Saudia, bado wamekataa kuwaachilia huru Wapalestina hao.
Gazeti la Lebanon la Al-Akhbar limemnukuu mmoja wa viongozi wa Harakati ya HAMAS akisema kuwa viongozi wa Saudia wamekataa kutoa jibu lolote kwa wapatanishi wanaoingia nchi hiyo kwa ajili ya kufuatilia suala la kutatuliwa faili la Wapalestina wanaoshikiliwa na Saudia. Kwa mujibu wa afisa huyo wa HAMAS, viongozi wa Saudia wanadai kuwa suala la mahabusu hao linahusiana na usalama wa ndani wa nchi hiyo.
Ni bora kuashiria kuwa wiki iliyopita Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Palestina HAMAS aliwasiliana na Saadeddine Othmani, Waziri Mkuu wa Morocco na kumtaka awe mpatanishi kuhusiana na suala la kuachiliwa huru Wapalestina wanaoshikiliwa na utawala wa Riyadh. Tangu mwaka jana, Saudi Arabia imewatia mbaroni zaidi ya Wapalestina na Wajordan 60 kwa tuhuma zinazohusiana na kuwa wanachama wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS).