Imran Khan: India inaangamiza kizazi cha Waislamu wa Kashmir
Waziri Mkuu wa Pakistan sambamba na kukosoa siasa za ukandamizaji za serikali ya India dhidi ya Waislamu, amesema kuwa hatua za New Delhi katika jimbo la Kashmir lililo chini ya udhibiti wa nchi hiyo ni za maangamizi ya kizazi.
Imran Khan aliyasema hayo Alkhamisi na kuitaka serikali ya India ihitimishe mauaji ya kizazi dhidi ya wakazi wa Kashmir yanayofanywa na askari na Wahindu wenye kufurutu ada wa nchi hiyo. Aidha Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kuwa, chama cha Bharatiya Janata (BJP) kinatumia vibaya suala la kuenea virusi vya Corona na karantini kuwakandamiza Waislamu wa nchi hiyo wakiwemo wale wa jimbo la Kashmir.
Imran Khan amezidi kubainisha kwamba, serikali ya Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India sambamba na kulifutia mamlaka eneo la Kashmir lililo chini ya India, kimsingi inatekeleza mabadiliko ya muundo wa kijamii wa eneo hilo jambo ambalo linakinzana wazi na sheria za kimataifa. Waziri Mkuu wa pakistan amesisitiza kuwa, hakuna nchi yenye haki ya kubadili muundo wa kijamii wa Kashmir hadi pale kutakapofanyika kura ya maoni. Sambamba na kuenea kwa virusi vya Corona nchini India baadhi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo vilieneza propaganda za chuki kwa kuwatuhumu Waislamu kuwa wahusika wa kuenea ugonjwa huo suala ambalo limechochea mashinikizo dhidi yao. Tangu ilipoingia madarakani serikali ya Narendra Modi, kumeshtadi mashambulizi ya maafisa usalama na Wahindu wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu wakiwemo wa eneo la Kashmir.