Mamluki wa Imarati wawashambulia kwa risasi waandamaji mjini Aden, Yemen
Mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu wamewashambulia kwa risasi watu waliokuwa wanaandamana mjini Aden, kusini mwa Yemen kulalamikia huduma mbovu za umma.
Duru za Yemen zimetangaza kuwa, wanamgambo na mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu ambao waeuteka na kuukalia kwa nguvu mji wa Aden wamewashambulia kwa risasi watu waliokuwa wanalalamikia kukosekana huduma za umma mjini humo, na ambao wamechoshwa na huduma mbovu za umma katika mji huo.
Mamluki hao wa Imarati aidha wamewatia mbaroni wanaharakati kadhaa waliotumia mitandao ya kijamii kuwahamasisha wananchi kufanya maandamano hayo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, yaani usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 26 Aprili 2020, wanamgambo wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wanaojiita Baraza la Mpito la Kusini (STC) walitangaza kuwa, kuanzia sasa watakuwa wanasimamia na kuendesha kivyao masuala ya mji wa bandari wa Aden na mikoa mingine ya kusini mwa nchi hiyo na walitangaza hali ya hatari katika maeneo hayo.
Uvamizi huo wa Imarati katika nchi nyingine unaendelea kulaaniwa hadi leo hii. Wakati huo, Muhammad Ali al Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ambaye ni katika viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Answarullah alilaani vikali kitendo hicho na aliiambia serikali iliyojiuzulu ya Abdu Rabbuh Mansour Hadi kwamba, nyinyi muda wote mumekuwa mukidai kuwa eneo la kusini mwa Yemen liko mikononi mwenu, haya sasa tekelezeni makubaliano chapwa ya Riyadh na wazuieni wanamgambo wa Imarati kujitangazia uhuru kusini mwa Yemen.