Wakati Saudia na Imarati zinapoitumia vibaya Sudan na baadaye kuiacha "solemba"
-
Vijana wa Sudan wanamwaga damu zao bila ya sababu nchini Yemen kwa tamaa ya ahadi za fedha za Saudia na Imarati kwa viongozi wa Sudan
Kwa muda sasa Sudan imebadilisha misimamo yake ya kisiasa kama njia ya kuvutia misaada ya kifedha kutoka kwa nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Saudi Arabia lakini nchi hizo hazioneshi utashi wowote wa kuitatulia Khartoum matatizo yake zaidi ya kuitumia tu kufanikishia malengo yao binafsi.
Mohamed Hamdan Dagalo, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan amekiri kwamba Saudi Arabia na Imarati hadi sasa hazijatekeleza ahadi zao za kuisaidia kifedha Sudan na kusema, hadi hivi sasa msaada wa fedha wa dola bilioni tatu ulioahidiwa na nchi hizo mbili kwa Sudan haujatolewa. Hii ni katika hali ambayo, Wasudan wengi wamemwaga damu zao huko Yemen na Libya kama sehemu ya kujipendekeza kwa Saudi Arabia na Imarati, lakini matokeo yake ni kuachwa njia panda na kufikia hadi hiyo ya viongozi wa Khartoum kulalamika kutopewa fedha walizoahidiwa na Riyadh na Abu Dhabi.
Mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini Sudan yalianza katika miaka ya mwishoni mwa utawala wa Jenerali Omar al Bashir ambaye aliingia tamaa ya kupata misaada ya kifedha kutoka kwa Imarati na Saudia, hivyo alifikia hadi kutuma wanajeshi wa Sudan kwenda kuuawa nchini Yemen ili kuzifurahisha nchi hizo mbili. Hali hiyo imeendelea hata baada ya kupinduliwa Omar al Bashir huko Sudan. Mbali na Saudi Arabia na Imarati, Misri nayo imejiingiza kwenye masuala ya Sudan kwa madai ya kulinda utulivu na iliahidi kuwapa misaada ya kifedha viongozi wa serikali ya mpito ya Khartoum lakini hakuna ahadi iliyotimizwa.
Kwa muda mrefu nchi mbili za Saudia na Imarati zinafanya juu chini, chini juu; kuhakikisha kuwa wimbi la kupigania demokrasia halipati nguvu katika ulimwengu wa Kiarabu kwani ni hatari kubwa kwa tawala za kurithishana za nchi hizo mbili. Nchi mbili za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilitangaza rasmi kuwa zitaipa Sudan msaada wa dola bilioni 3 lakini Naibu wa Mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan anasema hadi hivi sasa Khartoum imepokea hawala ya dola milioni 500 tu kutoka kwa nchi hizo mbili.
Wachambuzi wa mambo wanasema, kuendelea wanajeshi wa Sudan kushiriki katika vita vya kivamizi nchini Yemen, ndiyo sababu kuu inayozifanya Saudia na Imarati kuingilia masuala ya ndani ya Sudan na kufikia hata kuwarubuni kifedha viongozi wa Khartoum. Kwa kweli kuendelea kuweko wanajeshi wa Sudan huko Yemen chini ya mwavuli wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na Imarati kuna umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa wakuu wa nchi hizo mbili hasa Saudia na ndio maana zimeamua kuilaghai Khartoum kwa ahadi za mabilioni ya dola ili itume na ibakishe wanajeshi wake nchini Yemen.
Taarifa zinasema kuwa, kuna zaidi ya wanajeshi 30 elfu wa Sudan nchini Yemen na wengi wao ni watoto na vijana wadogo wadogo wanaokimbia maisha magumu nchini Sudan na ambao wako tayari kuhatarisha maisha yao kwa ahadi za kupewa fedha. Taarifa hizo zinasema, wengi wa watoto na vijana hao wanatoka eneo lililoathiribiwa vibaya na mapigano la Darfur, la magharibi mwa Sudan. Si hayo tu, lakini pia katika wiki za hivi karibuni zimepata nguvu taarifa za kuweko wanajeshi wa Sudan nchini Libya kwa amri ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kwa ajili ya kumsaidia jenerali muasi, Khalifa Haftar kuipiga vita Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa.
Ukweli ni kuwa kila mpenda haki duniani na kila mwenye fikra huru anawalaumu viongozi wa Sudan kwa kukubali kurubuniwa na kutuma vijana wa nchi hiyo kwenda kuuawa bure bilashi hasa huko nchini Yemen. Jamii ya kimataifa na wananchi, pamoja na vyama na makundi mengi ya kisiasa yanawalaumu viongozi wa Khartoum katika jambo hilo. Wananchi wengi Sudan wanasema, hawaoni sababu ya kwa nini vijana wao wanatumwa kwenye maeneo hatari huko Yemen na Libya kwa ajili ya kupigana kama mamluki wa Saudi Arabia na Imarati. Fat'hi Fadhl, mmoja wa wanaharakati wa Sudan anasema, suala haliishii tu kwenye ulazima wa kurejeshwa nyumba wanajeshi wa Sudan, bali suala muhimu zaidi ni kwamba Khartoum inapaswa kujitoa kwenye vita hivyo vya kiwendawazimu ambavyo lengo lake ni kutaka kulidhibiti taifa jingine, suala ambalo ni muhali kufanikiwa.
Kiujumla ni kwamba, inaonekana wazi kuwa, kushindwa Saudia na Imarati kutimiza ahadi zao kwa Khartoum kumezidi kuwaweka chini ya mashinikizo viongozi wa Sudan na kuwalazimisha walegeze misimamo yao kwa hofu ya kupoteza kikamilifu uungaji mkono wa wananchi. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, hatua ya Mohamed Hamdan Dagalo, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan ya kulalamika kuwa Saudi Arabia na Imarati zimeiacha "solemba" Khartoum imechukuliwa katika uwanja huo huo.