Jeshi la Iraq lamuua kiongozi wa ISIS nchini Syria
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, kiongozi mmoja mkubwa wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) ameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la Iraq katika maficho ya magaidi hao huko Deir ez-Zor, Syria.
Kwa mujibu wa televisheni hiyo, Jeshi la Anga la Iraq limeendesha operesheni ya kijeshi katika mkoa wa Deir ez-Zor wa mashariki mwa Syria na kumuangamiza Abou Ali al Ghazzawi, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa magaidi wa Daesh.
Gaidi huyo ndiye aliyekuwa mkuu wa masuala ya usalama ya genge la kigaidi la ISIS katika mikoa wa Baghdad na al Anbar nchini Iraq.
Taarifa zinasema kuwa, mbali na al Ghazzawi, kiongozi mwengine wa ISIS aliyekuwa amefuatana naye pia kuna uwezekano mkubwa ameangamizwa kwenye shambulizi hilo la anga.
Siku ya Jumanne pia, "Moataz Numan Abdel Nayef Najm al-Jabouri" naibu wa mkuu wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) aliyekuwa anaratibu mashambulizi ya kigaidi nje ya Iraq na Syria aliuawa katika shambulio la anga kwenye mkoa wa Deir ez-Zor mashariki mwa Syria.
Licha ya kushindwa magaidi wakufurishaji wa Daesh katika nchi za Iraq na Syria, lakini baadhi ya magaidi hao wamejificha ndani ya jamii za watu na katika maeneo tofauti ya nchi hizo mbili wakisubiri fursa yoyote ile wafanye mashambulizi ya kuvizia.
Kwa muda sasa vikosi vya ulinzi vya Iraq vimeanzisha operesheni pana na kubwa ya kupambana na magaidi ili kusafisha mabaki ya wanachama wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) lililoanzishwa, kusaidiwa, kupewa mafunzo na kuungwa mkono na madola ya kibeberu ya Magharibi hasa Marekani licha ya madola hayo hivi sasa kujifanya yameanzisha muungano wa kupambana na magaidi hao.